SERIKALI haijatoa ruhusa kwa Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee
kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya
kijamii.
Baadhi ya mitandao ilitoa taarifa yenye kichwa cha
habari kisemacho: “Waziri Mkuu
aruhusu kozi za 'Foundation' Chuo Kikuu Huria” kwa madai kuwa
alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwa mkoani
Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria
mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja
vya Kanisa Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu alisema Serikali bado inafanyia
maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.
“Kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani
sera tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze
kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” alisema.
“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia kufafanuliwa
kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea kuiboresha. Pindi
itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza
kushirikiana na sekta zote ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,”
alisema.
Mapema, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda alisema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa
kozi za Foundation katika chuo hicho.
“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi
matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri
mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” alisema
Prof. Bisanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, DESEMBA MOSI, 2017
No comments:
Post a Comment