HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 18, 2018

MADIWANI WATAKIWA KUTUNZA MIRADI YA MAENDELEO

 
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (katikati) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co. Ltd   (watatu kushoto), Premji  Pindoria wakati akikagua mtaro wa kutiririsha maji ya mvua uliyopo Mtoni kwa Azizi Ally ambao umejengwa na kamupuni hiyo.

Mtaro wa maji ya mvua uliyojengwa.
 
NA JANETH JOVIN 
 
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka madiwani wote nchini bila kujali vyama vyao kuhakikisha wanatunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata zao na kuwachukulia hatua mara moja watu wote wanaohujumu miundombinu hiyo. 
 
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miundombinu hiyo ikiwemo mifereji ili kuepukana na mafuriko yanayotokana na mvua.
 
Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya mitaro ya maji ya mvua katika mtaa wa Bungoni kata ya Buguruni na mtaa wa Miburani kata ya Mtoni ikiwa ni ziara yake ya siku mbili.
Alisema maendeleo ya nchi na athari za mabadiliko ya tabia nchi hayana vyama hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanatunza miradi hiyo na mazingira kwa ujumla. 
 
"Kuna athari kubwa kwa mambo tunayofanya wenyewe ikiwemo uharibifu wa mitaro, utiririshaji wa majitaka katika mitaro haswa kipindi cha mvua na kuathiri watoto wetu, kutuathiri sisi wenyewe na viumbe vinavyotuzunguka" alisema.
 
Alisema "kutiririsha kinyesi kwenye mitaro au kipindi cha mvua sio utamaduni wetu watanzania, hivyo naomba mitaro hii utumike kwa malengo yaliyokusudiwa... usafi ni nyumbani kwetu na mazingira yanayotuzunguka".
 
Aidha alisema "ni wajibu wa kila serikali kuhakikisha wananchi wake wanaishi salama na ndiyo sababu Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kujenga miradi ya maendeleo.Tuna wajibu wa kutunza usalama wenu ila pia usalama wako unaanza na wewe mwenyewe". 
 
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba alisema moja ya changamoto inayoikabili jiji la Dar es Salaam ni mafuriko ya mara kwa mara yanayosababishwa na uwepo wa miundombinu mibovu.
 
Hivyo Makamba amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia miundombinu hiyo iliyojengwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na si kwa kutiririsha maji machafu na kutupa taka.
"Tunajua mtaro huu wa buguruni na mingine iliyojengwa haitoshi kukabiliana na tatizo lililopo Dar es Salaam na ndio maana tunaendelea kuzungumza na wadau mbalimbali ili watupatie fedha tuweze kuboresha miundombinu yet, "alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages