WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema ameridhishwa na usafirishaji wa mbolea kutoka wa wasambazaji wa
pembejeo nchini kwenda kwa wakulima.
Pia ameitaka Kampuni ya Mbolea
Tanzania (TFC) kuwa na mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji wa mbolea
kwa wakati wote nchini.
Ametoa kauli hiyo leo
(Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akikagua usafirishaji wa mbolea kwenye
maghala makubwa matatu jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kuona
wakulima wote nchini wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea kwa wakati ili
kilimo kiweze kuwaletea tija.
Amesema TFC inatakiwa ianze maandalizi ya
usambazaji wa mbolea mapema kwani Serikali inataka wakulima wapate pembejeo
miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu.
Wakati
huo huo,
Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba akutane na wadau na
kufanya mapitio ya gharama za usafirishaji wa mbolea.
Amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha
mkulima aliyeko kijijini anapata mbolea
hiyo kwa gharama nafuu bila ya kumuathiri mfanyabiashara.
Pia amemtakaDkt. Tezeba ashirikiane na Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba ili kuhakikisha malori yanayobeba
mbolea yanafika katika mikoa husika kwa wakati.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa
Kilimo awasiliane na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbawala ili malori yanayobeba mbolea yakifika kwenye vituo vya mizani yapewe
kipaumbele.
“Si kwamba yaongeze uzito hapana, bali yapewe
kipaumbele cha kupima haraka ili yaweze kuwahisha mbolea kwa wakulima kwani
tayari msimu umeshaanza.”
Naye Waziri wa Kilimo, Dkt. Tizeba alisema
watahakikisha mbolea ya kutosha inakuwepo nchini na kwamba wakulima wote
wanaipata kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Maghala aliyoyakagua Waziri Mkuu ni ghala la
Mohammed Enterprises lililoko Mbagala, ghala la
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) lililoko Kurasini na ghala la Premium
lililoko Vingunguti ambako kote amekuta malori yakipakia mbolea kwa ajili ya uisafirisha
katika mikoa mbalimbali nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 10, 2018.
No comments:
Post a Comment