HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 09, 2018

Waziri Profesa Mbarawa avamia bandarini Usiku, abaini madudu

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa jana usiku amefanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini mawakala wa meli wanaotoa huduma katika bandari hiyo hawafanyi kazi saa 24 kama Serikali ilivyoelekeza.

Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa mawakala wote waliokiuka agizo la Serikali la kutoa huduma bandarini kwa saa 24.

"Kati ya Mawakala wa Meli nane ambao tumewatembelea usiku huu ni wakala mmoja tu ndiye tuliyemkuta akitoa huduma kwa saa 24 hivyo SUMATRA katika kipindi cha siku saba hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe kwa wote wanaokiuka utaratibu huu na nipewe ripoti ya hatua zilizochukuliwa," alisema Waziri Prof. Mbarawa.

"Katika ukaguzi huu tumegunduwa kuwa mawakala wengi wanaacha watoa huduma wasiostahili, wakiwemo walinzi kufanya kazi nyakati za usiku ambao hawawezi kutoa huduma inayostahili usiku na kuendelea kutoa huduma asubuhi jambo ambalo sio sahihi," amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali pamoja na benki, isipokuwa kwa taasisi ya Atomiki Enegy ambayo ameitaka ijieleze kwanini haifanyi kazi kwa saa 24 kama Serikali ilivyoagiza.

Profesa Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana bandarini hapo kwa ajili ya kuhudumia meli zinazoingia na kutoka na mapato yanayopatikana katika huduma hiyo ya maji kujulikana.

Waziri Mbarawa katika ziara yake ya kushtukiza aliambatana na maofisa wa SUMATRA ili kujionea wenyewe ukiukwaji wa agizo la Serikali na kusisitiza nia ya Serikali kuitaka Bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi saa 24 ni kuiwezesha kushindana na bandari nyingine katika ukanda wa Bahari ya Hindi na kuongeza mapato.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Giliadi Ngewe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza kwa simu na mmoja wa maofisa wa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kutembelea ofisini kwake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akiondoka katika eneo linalotolewa huduma za kibenki bandarini jana usiku mara baada ya kukagua kama huduma zinatolewa saa 24 kama Serikali ilivyoelekeza.

No comments:

Post a Comment

Pages