Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi mpya wa Tanzania nchini Urusi Meja Jenerali mstaafu Simon Marco Mumwi(kushoto) pamoja na Balozi mpya wa Tanzania nchini Rwanda IGP Mstaafu Ernest Mangu (kulia) mara baada ya hafla fupi ya uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi mpya wa Tanzania nchini Rwanda IGP Mstaafu Ernest Mangu akiwa katika picha na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro (wa kwanza kulia), Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala (wa kwanza kushoto), Mkuu wa Jeshi la Magereza Kamishna Jenerali wa Magereza Dk. Juma Malewa (wapili kutoka kulia) pamoja na viongozi wengine wa Jeshi la polisi mara baada ya hafla ya Uapisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Machi, 2018 amewaapisha Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi na IGP Mstaafu Ernest Jumbe Mangu kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Hafla ya kuwaapisha Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kuapishwa Mhe. Balozi Mumwi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kuwa katika kipindi chake atahakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaimarishwa na Tanzania inanufaika na uhusiano huo hususani katika azma yake ya kuvutia uwekezaji katika viwanda.
Kwa upande wake Mhe. Balozi Mangu pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini ameahidi kuongeza msukumo katika utekelezaji wa ajenda muhimu za maendeleo kati ya Tanzania na Rwanda hususani ujenzi na manufaa ya mradi mkubwa wa reli ya kati utakaoiunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi nne za magharibi mwa Tanzania ikiwemo Rwanda.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Dkt. Susan Kolimba amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda na ameahidi kuwa wizara hiyo itakuwa tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo diplomasia ya uchumi.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Mabalozi hao kufuatilia na kusimamia kwa ukaribu makubaliano mbalimbali ambayo Tanzania na nchi hizo wameyafikia ikiwemo miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Millicom International Services LLC inayomiliki kampuni ya simu za mkononi ya Tigo Bw. Mauricio Ramos, Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumza kuhusu uwekezaji wa kampuni hiyo hapa nchini.
Baada ya mazungumzo hayo Bw. Mauricio Ramos amesema amekuja kumweleza Mhe. Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya kampuni hiyo ambayo imewekeza Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 1 (sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 2.23 za Tanzania) katika miaka mitano iliyopita, imeajiri wafanyakazi zaidi ya 90,000 na kuwafikishia mawasiliano Watanzania kwa takribani asilimia 90.
Bw. Mauricio Ramos amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada zake za kupambana na rushwa na amebainisha kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo na kupunguza umasikini.
Nae Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ni ya pili kwa ukubwa hapa nchini ikiwa na wateja Milioni 11.06 na imekuwa ikilipa vizuri kodi ambapo mwaka 2017 ililipa kiasi cha Shilingi Bilioni 262.77.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na watendaji wakuu wa kampuni ya Ferrostaal kutoka nchini Ujerumani na Denmark na Watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Nishati, ambapo wamejadili kuhusu mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea Mkoani Lindi.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani na Balozi wa Denmark hapa nchini Mhe. Einar Hebogard Jensen.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Machi, 2018
No comments:
Post a Comment