May 02, 2018

UBONGO LEARNING YAKABILIANA NA UWEZO WA VIJANA WA KITANZANIA KUPATA AJIRA

Ubongo Learning ambalo ni shirika linaloongoza barani Afrika kwa maudhui ya elimu ya kuburudisha kwa watoto, leo imeandaa mkutano wake wa mwaka ambao ulikuwa na lengo ya kuzungumzia uwezeshwaji kiuchumi, haswa kwa wasichana ambao wanaweza kuathirika zaidi ya wavulana kutokana na mabadiliko katika soko la ajira.

Kwa kipindi cha miezi 6 sasa, Ubongo Learning, shirika lisilo la kibiashara ambalo ndiyo lilibuni katuni za kuelimisha za Ubongo Kids, limekuwa likifanya utafiti juu ya uwezo wa kupata ajira na usimamizi wa fedha miongoni mwa vijana nchini Tanzania. 

Lengo la mradi huu, uliofadhiliwa na Data for Local Impact (DLI), ni kuelimisha vijana, haswa wasichana jinsi ya kutumia maelezo, taarifa na takwimu zinazopatikana ili kufanya maamuzi bora juu ya maisha yao ya mbeleni, na zaidi ya hilo kupitia ujuzi wa masala ya kifedha. Vipindi vya televisheni vya Ubongo vinatazamwa na zaidi ya watu milioni 6.4 kila mwezi, hivyo kuvifanya kuwa vipindi vya watoto vyenye watazamaji wengi kuliko vyote Afrika Mashariki na kuwa sehemu nzuri sana kuwasilisha maswala muhimu kwa vijana.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano huo, Meneja Masoko Ubongo Learning Iman Lipumba alisema licha ya kuwa na Maendeleo makubwa ya kuhakikisha wasichana wanaandikishwa shule za msingi, lakini bado jamii nyingi nchini Tanzania bado zinawapendelea wavulana kielimu (hususan kwenye elimu ya shule za sekondari na vyuo vikuu) zaidi ya wasichana. Zaidi ya hilo, utafiti wetu unaonyesha kuwa wavulana wanashawishiwa zaidi kusoma masomo ya sayansi, hesabu na ukandarasi, taaluma ambazo zinahitajika sana katika soko la ajira, na wasichana wanashauriwa kuingia kwenye masomo ya sanaa na hatimaye kufanya kazi za utoa huduma ambazo huenda zikapotea katika miaka michache ijayo.
‘Tunahitaji kubadilisha hali hii. Sisi tunaamini kuwa kama vijana watapatiwa maelezo na taarifa hizi tangu awali, itawasaidia kufanya maamuzi bora kitaaluma ili kujaza nafasi zinazoongezeka kweney soko la ajira nchini Tanzania’ alisema Lipumba.

Kwa miaka 10 iliyopita, stashahada ya sheria au digrii yoyote nyingine kutoka chuo kikuu ingemhakikishia kijana kazi bora. Lakini, katika dunia ya leo, mabadiliko ya kasi kubwa katika teknolojia yamebadilisha kabisa maisha yetu, haswa jinsi tunavyofanya kazi. 

Wakati ajira katika taaluma zilizozoeleka kama vile sheria, utawala na biashara zinapungua, fursa za ajira katika IT, ukandarasi na kazi za kisanii kama vile kuendesha masoko kidijitali zinaongezeka kwa kasi kubwa sana. Tena, asili mia 65 ya watoto wanaoanza shule za msingi leo watakuja kuingia kwenye taaluma au kazi ambazo hazijawahi kuwepo kabisa.

 Hivyo, Ubongo Learning inajishughulisha na kuwawezesha vijana wa Tanzania kuwa na vipaji vitakavyohitajika ili kuwa na mafanikio katika mazingira yenye kasi na kutokuwa na uhakika wa mabadiliko yajayo. Aliongeza Lipumba. 

Likiwa shirika lisilo la kibiashara, Ubongo Learning linaanda maudhui ya kielimu ya kufurahisha na yenye kulenga na kuendana na maeneo au nchi maalum, maudhui ambayo yanawasadia watoto kujifunza na kutumia mafunzo hayo kubadilisha maisha yao. Shirika linafikia mamilioni ya familia barani Afrika kupitia teknolojia zinazopatikana kirahisi kama vile televisheni, redio na simu za mkononi.

Vile vile, Ubongo Learning imetengeneza katuni zinazofundisha vijana taaluma nyingine zenye thamani kubwa kama vile kuandika programu za kompyuta, jinsi ya kuhakiki taarifa za mtandaoni pamoja na utunzaji akiba, kupanga matumizi na kujipatia kipato. Pia tunafanya kazi na wadau wengine kama vile DLI amabo nao wanajishughulisha na kuelimisha vijana ili kuwapatia vipaji mbali mbali kuwawezesha kupata mafanikio.

No comments:

Post a Comment

Pages