*Achangisha
mifuko 2,000 ya saruji ujenzi wa uzio wa sekondari
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechangisha
mifuko 2,000 ya saruji na sh. milioni 50 kwenye harambee ya papo kwa papo kwa
ajili ya ujenzi wa uzio wa sekondari ya Mwendakulima wilayani Kahama.
Waziri Mkuu ameendesha zoezi hilo
leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati
akizungumza na walimu na wanafunzi wa sekondari ya Mwendakulima, wilayani
Kahama mkoani Shinyanga ambako alienda kupokea mabweni mawili ya wasichana.
Ujenzi wa mabweni hayo yenye uwezo wa kulaza
wanafunzi 126, umegharimu sh. milioni 560 na umefadhiliwa na kampuni kuchimba madini
ya ACACIA kupitia fedha za Corporate
Social Responsibility. Mabweni ya awali yaliteketea kwa moto.
Waziri Mkuu ameendesha harambee hiyo baada ya
kuombwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwendakulima, Bi. Neema Mfunya. Kwa
wastani, mfuko mmoja wa saruji unagharimu sh. 16,500.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu alichangaia mifuko
500 ya saruji, huku kampuni ya ACACIA ikichangia mifuko 400 kutoka kwa
watumishi wake. MNEC wa Simiyu, Bw. Emmanuel Nsangali aliahidi kuchangia mifuko
200.
Ahadi nyingine zilizotolewa na Naibu Mawaziri,
wabunge, na wakuu wa taasisi waliombatana na Waziri Mkuu kwenye ziara yake
zilikuwa ni za mifuko 50 hadi 100.
Shule ya sekondari ya Mwendakulima ina wanafunzi 336
wa kidato cha tano na cha sita. Lakini kwenye kidato cha kwanza hadi cha nne,
shule hiyo ina wanafunzi 771 ambao kati yao, wavulana ni 423 na wasichana ni
348.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.
No comments:
Post a Comment