WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
kesho (Jumatano,
Julai 25, 2018) anatarajiwa kushiriki zoezi za usafi eneo la Coco Beach pamoja
na wananchi na watendaji mbalimbali.
Zoezi hilo ni utekelezaji wa
agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
alilolitoa Juni 29 mwaka huu kwamba Watanzania wafanye usafi kwenye maeneo yao ikiwa
ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa
ambayo huadhimishwa Julai 25, kila mwaka.
Kwa
muhibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, wananchi
wanatakiwa wafike eneo hilo kuanzia saa 12:30 asubuhi ili waanze shughuli hiyo.
Usafi huo utafanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea
maeneo ya Police Officers’ Mess.
Juni
29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha
polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Rais Dkt Magufuli anawataka Watanzania
wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo
yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni
njia ya kuwaenzi.
Siku
hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh.
milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Aliitaja
miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari katika barabara ya Kisasa
na taa za barabarani kwenye barabara mpya ya kutoka Emmaus hadi African Dream
yenye urefu wa kilomita 1.4, ambayo kwa sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JULAI
24, 2018.
No comments:
Post a Comment