Na Mwandishi Wetu
BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo
Bw. Richard Mayongela kwa kuthibitishwa rasmi katika nafasi hiyo.
Awali Bw. Mayongela alikuwa akikaimu
nafasi hiyo kwa takribani miezi 11 iliyopita.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti
wa MAB, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema kwa niaba ya bodi nzima amesema
"Nimepokea taarifa rasmi ya kuthibitishwa kwako kuwa Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania. Ninakupongeza."
Mhandisi Prof. Lema amesema kutokana na
wadhifa huo, anatumaini makubwa Mkurugenzi huyo ataendelea kuiongoza Mamlaka hiyo
kwa utendaji makini na kwa weledi wa hali ya juu unaozingatia ufanisi na
uadilifu usio na shaka yoyote.
Pia amemtaka Bw. Mayongela kujenga timu
yenye nguvu kwenye Mamlaka itakayoongozwa kwa misingi ya dira
sahihi na mwelekeo mmoja kwa wote, unaoheshimu na kuzitumia fani za
kila mtumishi wa Mamlaka ipasavyo kwa manufaa mapana ya Taifa.
"Mungu akuzidishie hekima katika
majukumu yako," amesema Mhandisi Prof. Lema.
Uthibitisho huo uliwasilishwa na Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Issac Kamwelwe na kusomwa katika
mkutano wa Mameneja wa Viwanja vya Ndege Tanzania uliofanyika hivi
karibuni Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na
Utawala, Bw. Lawrence Thobias.
Halikadhalika, Bw. Mayongela baada ya
uthibitisho huo rasmi aliwashukuru
Watumishi wote wa Mamlaka na kusema
hatua hiyo imechangiwa na juhudi za pamoja na ushirikiano kwa kipindi chote cha
takribani miezi 11 alichokuwa akikaimu nafasi hiyo.
"Bila nyie nisingeweza kufanya
kitu chochote, na hali kadhalika bila ushirikiano wenu peke yangu
nisingeweza," amesema Bw. Mayongela.
Hatahivyo amewasisitizia Watumishi
wenzake kuchapa kazi kwa weledi, bidii, maarifa na uzalendo mkubwa usioweza
kutiliwa mashaka ya aina yoyote kwa kuwahudumia Wadau na Watanzania wote kwa
ujumla ili kuleta tija kubwa kwa taifa.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA MAWASILIANO MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)
No comments:
Post a Comment