NA MWANDISHI WETU, TABORA
SHAHIDI wa nane katika shauri la Uhujumu linalowakabili vigogo wa Ushirika wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) Goodluck
Amos ameiambia Mahakama kuwa taratibu za manunuzi ya gari aina ya
Toyota V8 hazikufuatwa.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Tabora,
Chiganga Mashauri, shahidi huyo ambaye kwa sasa ndiye Mhasibu Mkuu wa Ushirika
huo alisema mchakato wa manunuzi ya gari hilo ulianza kabla ya kikao cha Bodi.
Huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro,
shahidi huyo alisema kuwa bodi ya Wetcu ilikutana tarehe 30 Juni mwaka 2015 na
kuiagiza Menejimenti ianze mchakato wa kupata
Kampuni itakayoweza kuiuzia gari WETCU.
Amos alisema kuwa Hati za nukuu ya bei (quotation) toka
makampuni mbalimbali ziliandaliwa kati ya tarehe 21 na 24 Juni mwaka 2015
huku kikao cha Bodi kuidhinisha kuanza mchakato wa manunuzi ulifanyika tarehe
30 Juni mwaka 2015.
Aliongeza kuwa kinachoonyesha taratibu hizo zilikiukwa ni
pale Bodi ilipoagiza kuandaa taratibu za kawaida za
ununuzi wa gari aina ya Toyota V8 huku ikielekeza ipewe Kampuni ya Tanzania 4 x
4 LTD.
Katika kudhihirisha ukweli huo shahidi huyo alitoa
Nyaraka hizo kutoka kampuni za Betomotors
Tz Limited, Jan Motors Ltd na ile ya Tanzania 4X4 Ltd zote zikiwa na
bei tofauti kitendo kinachoonyesha kuwa mchakato huo
ulivyoanza mapema kabla ya kikao cha bodi.
Shahidi mwingine Deogratias Rugangira
aliiambia Mahakama hiyo kuwa maamuzi ya mkutano mkuu wa Ushirika huo yaliagiza
kuwa fedha zitakopatikana kutokana na uuzaji wa hisa zitumike kulipia baadhi ya
madeni waliyokuwa wanadaiwa.
Rugangira ambaye ni Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika
nchini alisema kuwa kitendo cha watuhumiwa kutumia fedha hizo kununulia gari ni
kosa kwa mujibu wa sheria za vyama vya ushirika.
Aliongeza kuwa maamuzi ya mkutano mkuu yanatakiwa yaheshimiwe na
Bodi pamoja na menejimenti kwani kazi yao ni kutekeleza matakwa ya wanaounda
ushirika huo ambao ni vyama vya msingi vya ushirika.
Watuhumiwa wa shauri hilo la kuhujumu uchumi namba 2/2017 ni
Gabriel Mkandala, John Kusaja, Prosper Mbacho, Hamza Kapera, Fransis Penta,
Msafiri Said na mfanyabiashara Faras Yassin Abbas.
Shauri hilio litaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo kwa upande
wa Jamuhuri kuendelea kuleta mashahidi wake.
No comments:
Post a Comment