*Ameimarisha nidhamu, uadilifu kwenye utumishi wa umma
*Ameboresha miundombinu ya reli, barabara, nishati, elimu na afya
WAZIRI MKUUKassim Majaliwa
amesema Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu ya
uongozi wake, amefanikiwa kuimarisha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji
ndani ya utumishi wa umma pamoja, kukemea uzembe na kujenga ari ya kufanya kazi.
Mafanikio
mengine ni ununuzi wa meli katika ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria
pamoja na kufufua Shirika la Ndege la Tanzania ili kuimarisha usafiri wa
anga na kukuza sekta mtambuka zikiwemo za utalii, afya, kilimo na
kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (SGR).
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 14, 2018) wakati akiahirisha
mkutano wa 12 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi
Novema 6, 2018.
Amesema mafanikio mengine yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Magufuli ni kuendesha
vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma sambamba na
kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za
nchi ikiwemo madini na maliasili.
“Kujenga vyanzo vipya vya umeme kama vile mradi wa kuzalisha umeme wa maji megawati 2,100 katika bonde la mto Rufiji (Stiegler’s Gorge),
kusambaza umeme hadi vijijini sambamba na kuongeza kasi ya utekelezaji
wa miradi ya awamu ya tatu ya mpango wa REA ujenzi wa mradi wa bomba la
mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania).”
Waziri
Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ameimarisha huduma za afya hususan
upatikanaji wa dawa, vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya
pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya na utoaji
Elimumsingi Bila Malipo kwa watoto wa Kitanzania.
Pia
amehakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa inakuwa bora, yenye
uwiano na thamani halisi ya fedha pamoja na kukamilishwa kwa wakati na
kuimarisha kilimo, ushirika na bei za mazao ya biashara.
Waziri
Mkuu amesema juhudi zote hizo zinafanywa kwa lengo la kuiwezesha nchi
kufikia malengo ya dira ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa
na viwanda ifikapo mwaka 2025. “Niwaombe Watanzania wenzangu tuendelee
kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kuleta maendeleo.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa ya uwepo wa
mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, biashara na upatikanaji wa
malighafi kwa kuja kujenga viwanda mbalimbali hususan vya kuchakata
mazao ya kilimo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
IJUMAA, SEPTEMBA14, 2018.
No comments:
Post a Comment