*Wakuu
wa Mikoa iliyobakia waagizwa ‘wakaze buti’
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi sasa mikoa
14 imeanza kutekeleza kampeni ya kitaifa ya kupima VVU kwa hiari pamoja na
kuanza mapema matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARV) kwa wale
watakaogundulika kuwa na maambukizo.
Amesema hadi kufikia Septemba 2018, mikoa ya Arusha,
Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kigoma na Manyara imeanza kutekeleza kampuni
hiyo. Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Mbeya, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma,
Shinyanga, Tabora na Tanga.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa,
Septemba 14, 2018) katika hotuba yake
aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, mwaka huu.
Amewataka Wakuu wa Mikoa
ambayo bado haijaanza kutekeleza kampeni hiyo waanze mara moja. “Kwa kutambua
umuhimu wa kampeni hii, ifikapo Desemba mosi, 2018 wakati wa kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani tutafanya tathmini ya utekelezaji kwa
mikoa yote nchini. Kwa msingi huo, nisisitize wadau wote wenye mapenzi mema na
nchi hii wasaidie katika utekelezaji wa kampeni hiyo.”
Ametumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Mikoa hiyo 14 na akawataka waendelee
kuhimiza wananchi waliopo kwenye maeneo yao hasa wanaume wawe tayari kutambua
afya zao kuhusu maambukizo ya VVU kupitia kampeni hiyo.
Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu alizindua
kampeni ya kitaifa ya kupima kwa hiari VVU jijini Dodoma ijulikanayo kama “FURAHA YANGU, PIMA, JITAMBUE, ISHI” ambayo
imewalenga Watanzania wote kujitokeza kupima na kutambua afya zao hususan
wanaume ambao hawajitokezi kwa wingi kupima na kutambua afya zao.
“Wanaume wengi
tumekuwa tukiwatumia wenza wetu kutambua kama tumeathirika au la. Tunakaa
majumbani tunasubiri tu, ukimuona mwenza wako anarejea kutoka kliniki akiwa mwenye
furaha na wewe unajipa matumaini kuwa umesalimika. Sasa wanaume wenzangu tubadilike,
tuanze kuchukua hatua za kupima na kutambua afya zetu,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali
inafanya juhudi za kuhamasisha kampeni hiyo kupitia kwenye Ligi Kuu ya Mpira wa
Miguu Tanzania Bara kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
“Tunafanya hivyo
kwa kutambua kuwa Mpira wa Miguu ni mchezo unaoongoza kwa kupendwa duniani na
Tanzania. Aidha, kufuatia hatua ya kituo cha matangazo ya televisheni cha AZAM kuamua
kuonesha ligi yetu, watu wengi wamepata mwamko wa kutazama na kufuatilia
michezo ya Ligi kuu ya Tanzania. Hivyo, tuna uhakika wa kuwafikia wananchi
wengi na kuwahamasisha kuchukua hatua za kupima VVU na wale watakaogundulika
kuwa na maambukizo waanze mapema matumizi ya ARV.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA,
SEPTEMBA 14, 2018.
No comments:
Post a Comment