WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imedhamiria kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta ili Tanzania iachane na uagizaji wa mafuta ya kula
kutoka nje.
Amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha
kuwa mkoa wa Kigoma na maeneo mengine yenye fursa ya kulima zao la chikichi
yanaimarisha kilimo hicho. “Hivi sasa, nchi yetu inatumia takribani Dola za
Marekani milioni 294 kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta hayo.”
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba
14, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, mwaka huu.
Amesema sambamba na azma ya Serikali ya kuweka
mkazo katika kusimamia uzalishaji na masoko ya mazao makuu matano ya biashara
ambayo ni pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku, Serikali imedhamiria pia kupanua
wigo kwenye mazao mengine muhimu ikiwemo chikichi, alizeti na ufuta ili kukidhi
uzalishaji wa mbegu za mafuta nchini.
“Katika
kutekeleza azma ya Serikali, kuhusu kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula
nchini, tarehe 28 Agosti, 2018 nikiwa mkoani Kigoma nilizindua kampeni maalumu
ya kuendeleza zao la chikichi ambalo kwa sasa linatambulika kama zao kuu la
sita la kipaumbele,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa
mahitaji ya mafuta ya kula, Serikali
imeweka mikakati ya kuendeleza zao la chikichi kwa kuanzisha kituo cha utafiti wa
zao la chikichi katika eneo la Kihinga, mkoani Kigoma.
“Serikali imeandaa mpango
mkakati wa uzalishaji wa miche bora ya chikichi milioni 20 ifikapo mwaka 2021.
Kwa kuanzia, mwaka 2018/2019, Serikali inakusudia kuzalisha miche bora ya
chikichi milioni 10 ambayo itasambazwa kwa wakulima,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali
pia imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano wa utafiti wa mbegu bora ili
kuongeza tija kutoka tani 1.6 hadi kufikia tani 4.0 za matunda ya chikichi kwa
hekta kwa mwaka.
Amesema Serikali
imeweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na matumizi ya teknolojia ya kisasa
kwa ajili ya uchakataji zao la chikichi na imepanga kusimamia vituo vikuu vya
uzalishaji vya gereza la Kwitanga, Ilagala na JKT Bulombora.
Amewataka Watanzania
wachangamkie
fursa ya kilimo cha zao la chikichi ili nchi
iweze
kujitosheleza kwa mafuta ya kula na ziada kuuza nje. “Nitoe rai pia kwa
wawekezaji, waje kuanzisha viwanda vya kuchakata chikichi na
mazao yake,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amesema Serikali kwa upande wake, inaimarisha
taratibu za uingizaji wa sukari na mafuta ya kula kwa kuweka madaraja na
usimamizi makini.
Ameitaka Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wakamilisha jukumu
hilo kwa wakati.
“Pia, naagiza vyombo vya dola viongeze ushirikiano na mamlaka husika ambazo ni TRA, TFDA, Bodi ya Sukari na TBS ili kudhibiti uingizaji holela wa sukari na mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya magendo,” amesema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA,
SEPTEMBA 14, 2018.
No comments:
Post a Comment