Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Bondia Hassan Mwakinyo
kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma Septemba 14, 2018. Mwanamasumbwi
huyo hivi karibuni alimtwanga kwa TKO, Bondia Sam Egginton wa Uingereza
katika pambano lililofanyika Birmingham. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
WAZIRI MKUUKassim Majaliwa amempongeza mwanamasumbwi wa Kitanzania Bw. Hassan Mwakinyo (23) kwa kumchapa bkondia Mwingereza Bw. Sam Egginton.
Bw. Mwakinyo alimchapa Bw Egginton kwenye raundi ya pili ya pambano lao la masumbwi lililofanyika Jumapili, Septemba 9, 2018, huko Birmingham nchini Uingereza.
Waziri
Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Ijumaa, Septemba 14, 2018) wakati
akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge
limeahirishwa hadi Novemba 6, 2018.
Amesema
bondia huyo amelipa Taifa heshima kubwa kwa kulitangaza kimataifa
katika Nyanja ya michezo, hivyo amewataka wanamichezo wengine nchini
waige mfano wake.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake (Kilimanjaro Queens) kwa kutwaa kombe la Afrika Mashariki.
Pia ameipongeza timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
kwa kuwa washindi wa tatu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwenye
mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
“Hongereni sana wanamichezo wetu na endelezeni moyo huo wa kizalendo mliouonesha katika kulitangaza Taifa letu.
Pia
Waziri Mkuu amesema mwaka 2019 Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano
ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON-U17)
yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.
Amesema
hiyo ni fursa nyingine ya kipekee ya kulitangaza Taifa letu katika
nyanja za Kimataifa, hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
inaendelea na maandalizi, ambayo yatahusisha ukarabati wa viwanja
vitakavyotumika katika mashindano hayo.
Waziri
Mkuu ametoa wito kwa wananchi watumie vizuri uwepo wa mashindano hayo
kujiongezea kipato hususan kupitia biashara ya bidhaa na huduma kwa
wageni, pia amewataka wawe wazalendo kwa kuunga mkono timu zinazoshiriki
mashindano ya Kimataifa ili zipate mafanikio.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
IJUMAA, SEPTEMBA14, 2018.
No comments:
Post a Comment