HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 18, 2018

TAA Yawasilisha Tozo ya Abiria kwa Waendeshaji wa Mashirika ya Ndege

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati) jana akijadili jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara, Bw. Pius Wankali (kulia) na Kaimu Meneja Mipango na Takwimu, Bw. Nasib Elias (mwenye fulana ya bluu bahari) kabla ya mkutano na Wendeshaji wa Mashirika ya ndege kuanza kwenye ukumbi wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Myerere (JNIA-TB2). Kushoto ni Kaimu Mwanasheria wa TAA, Bw. Elius Mwashiuya.
 Meneja Uwajibikaji wa Shirika la ndege la Safari Plus LTD, Bw. Lauriano Balilemwa jana akitoa mapendekezo kwa ajili ya maboresho ya tozo ya usalama wa abiria wakati wa mkutano ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Waendeshaji wa mashirika ya ndege zinazofanya safari kuanzia kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
 Waendeshaji wa Mashirika ya Ndege zinazofanya safari zake kwa kuanzia kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati mbele) jana alipozungumza nao kuhusiana na tozo ya usalama wa abiria ambayo itaanza rasmi kutumika Oktoba 1, 2018.
 Bw. Sammy Ndiramgu (kushoto) jana akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela baada ya kumalizika kwa mkutano na Waendeshaji wa Mashirika ya ndege uliofanyika kwenye ukumbi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
 Mwenyekiti wa Waendeshaji wa mashirika ya ndege ndogo za abiria, Chief Uyeka Rumbyambya akitoa mapendekezo kwa ajili ya maboresho wakati wa kikao kati ya uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na waendeshaji hao uliofanyika jana kwenye Jengo la Pili la abiria la Julius Nyerere (JNIA-TB II).

   
Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), jana imewataarifu Waendeshaji wa Mashirika ya ndege za abiria zinazofanya safari zake kuanzia kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) juu ya tozo mpya ya usalama wa abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amewaeleza kuwa utekelezaji wa tozo hiyo ambayo ni dola tano (5) kwa abiria wan je ya nchi na abiria wa ndani ni sh. 5,000 utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba, 2018.

Bw. Mayongela amesema lengo la tozo hiyo ni uboreshwaji wa huduma na miundombinu ya Usalama katika Viwanja vya Ndege nchini ili kuhakikisha vinafikia viwango vya ubora vya Kimataifa na pia kutoa huduma bora za kiusalama kwa wadau wake.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na ada hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa TAA, Bw. Pius Wankali ameeleza kwamba agizo la ukusanywaji wa tozo  hiyo ulitangazwa rasmi na Mamlaka ya Usafiri wa  Anga (TCAA) mwezi Juni mwaka huu.

“Tangazo la kuanzishwa kwa tozo hii lilichapishwa na TCAA kutoka kwenye nyaraka AIC Doc No. TCAA/FRM/ANS/AIS-30, tarehe 29 Juni, 2018 na utekelezaji wake utakuwa ni kuanzia Oktoba Mosi, 2018," amesema Bw. Wankali.

Kwa upande wa wawakilishi wa mashirika ya ndege kubwa kutoka Shirika la ndege Tanzania (ATCL), Bw. Ismail Ismail alitaka kuwepo kwa maelezo ya kina juu ya tozo hiyo, ambayo alitaka ijumuishwe ndani ya tiketi ili abiria awe ameilipia moja kwa moja.

Kwa upande wake mwakilishi mwingine wa ndege kubwa ya KLM, Bw. Alexander Van de Wint ameomba tozo hii ianze baadaye mwakani kutokana na wao tayari wameshauza tiketi za msimu hadi Desemba 2018 ili wasiwaumize abiria wao.

Mwenyekiti wa Waendeshaji wa Ndege ndogo za abiria, Chief Uyeka Rumbyambya amesema kuwe na taratibu za kumuhusisha Mkurugenzi Mkuu katika mikutano mbalimbali ya Waendeshaji wa Mashirika ya ndege, ili waweze kuwasilisha.

Naye Kaimu Meneja Mipango na Takwimu wa TAA, ambaye ni mratibu wa mkutano huo, Bw. Nasib Elias alitoa ufafanuzi juu ya ukusanywaji wa tozo hii, ambayo inatarajiwa pia kuwa ni moja ya chanzo cha mapato cha Mamlaka.

No comments:

Post a Comment

Pages