KUMEIBUKA matangazo kwenye mtandao wa FACEBOOK
yanayosema kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki sherehe ya uzinduzi wa
tovuti ya www.boreshamaisha.ml ambayo
inatoa mikopo ndani ya dakika 45.
Waliofungua ukurasa huo wa FACECOOK, hawana
uhusiano wowote na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tovuti hii ya www.boreshamaisha.ml inaonesha ni ya
Malaysia wala siyo ya Tanzania. Wanasema wanatoa mikopo hiyo kutoka mfuko wa VICOBA TANZANIA
ambao umeanzishwa katika mfumo wa intaneti pekee (online). Wanadai wanatumia
mawasiliano ya teknolojia kwa uchukuzi wa haraka kupitia tovuti kwa lengo la
kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa kila Mtanzania popote alipo.
Wafunguaji wa akaunti hiyo, wametumia jina la
Kassim Majaliwa na wameweka picha yake akiwa Bungeni. Wanadai kwamba Waziri
Mkuu alipokea barua kutoka vyama vya upinzani wakilalamika kwamba utoaji wa
mikopo hiyo online kutoka kwenye mfuko wa VICOBA TANZANIA ni rushwa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Pia wanadai kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu
pamoja na viongozi wengine wamechangia fedha zao kwenye mfuko huo wa kijamii
unaolenga kuwapatia Watanzania wote mikopo bila ubaguzi wa aina yoyote kwamba
alishiriki uzinduzi wa tovuti hiyo.
Kwa taarifa hii ya umma, tunapenda kuujulisha umma wa Watanzania kwamba Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa hajashiriki uzinduzi wa tovuti hiyo, hana uhusiano wowote na watu hao
na wala hana akaunti ya facebook inayohamasisha Watanzania wapate mikopo kwa
dakika 45 kupitia njia ya mtandao.
Tunawaomba Watanzania wajiepushe na akaunti
hiyo ya FACEBOOK kwa kuwa si halali na haina nia njema kwa watumiaji. Aidha, hiyo
si akaunti ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wala Ofisi ya Waziri Mkuu
haijawahi kuunda akaunti ya mtandao yenye jina lake kwa matumizi yake binafsi
au ya ofisi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, SEPTEMBA 19, 2018.
No comments:
Post a Comment