HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 12, 2018

FUKWE KUIMARISHWA NA KUWA KIVUTIO CHA UTALII-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamesema Serikali itaweka mikakati madhubuti kwa lengo la kuimarisha matumizi ya fukwe kama sehemu ya kivutio cha utalii ili kongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini na kutengeneza ajira kwa wananchi sambamaba na kukuza uchumi wa Taifa.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba 12, 2018) wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye ufunguzi wa onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo, katika  Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar ES Salaam.

Onesho hilo linalofanyika kwa siku tatu nchini linahudhuriwa na wafanyabishara wakubwa wa utalii takriban 170  kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wauzaji wa bidhaa za utalii takriban 300 kutoka ndani na nje ya nchi.

Waziri Mkuu amesema sekta ya utalii nchini inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na takriban ajira 1,500,000, ambapo kati ya ajira zote za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja.

Amesema kutokana na juhudi za utangazaji wa vivutio vya utalii nchini unaoratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wageni wengi maarufu duniani wanakuja kuona vivutio hivyo wakijua kwamba Tanzania ni nchi ya amani, yenye utulivu na Watanzania ni watu wakarimu. 

Amsema kati ya wageni hao waliokuja hapa nchini kwa mwaka huu ni pamoja Rais Mstaafu wa Marekani, Bw. Barack Obama aliyekaa siku nane; Rais wa Uswisi Bw. Alain Berset aliyekaa siku 10 pamoja na mchezaji wa golf mstaafu kutoka Marekani, Bw. Jack Nicklaus.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa  mbali na watu hao maarufu duniani kuja nchini pia makundi makubwa ya watalii yenye zaidi ya watu 300, wameingia nchini tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutoka nchi za Israel, Australia na Hispania. “Hii ni ishara njema kwa maendeleo ya kasi ya sekta hii.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya sekta ya utalii nchini kutokana na hatua mbalimbali anazozichukua katika kukuza sekta hiyo.

Amesema miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli katika kuimarisha sekta ya utalii ni pamoja na kuboresha usafiri wa anga nchini, ambao kwa sasa umeongezeka kwa sababu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali.

“Ununuzi wa ndege saba mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ambapo ndege nne tayari zimeshawasili na kuanza kutoa huduma ni kielelezo tosha cha juhudi za Serikali. Kati ya ndege hizi zipo ambazo hivi karibuni zitaanza kutoa huduma ya usafiri kati ya Tanzania na nchi za India na China.”

Waziri Mkuu ametaja hatua nyingine kuwa ni ujenzi wa jengo la abiria yaani “Terminal 3”kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo baada ya kukamilika na kuanza kutumika jengo hilo linatarajiwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa kwa abiria na kuruhusu ndege nyingi zaidi kuingia na kutoka nchini. Ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 12, 201

No comments:

Post a Comment

Pages