*Atoa miezi miwili Wizara ya Habari ikamilishe mchakato wa vazi la Taifa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa muda wa miezi miwili na nusu kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezoiwe imekamilisha mchakato wa Tanzania kuwa na vazi la Taifa.
Amesema
Watanzania bado hawajaunganishwa kwa kuwa na vazi la Taifa, ambalo
mchakato wake umeendeshwa kwa miaka mingi na wizara hiyo bila ya
kujulikana wamefikia wapi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Oktoba 13, 2018) wakati akifunga tamasha za Urithi Festival, lililofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
“Ifikapo
Desemba 30,2018 tuwe tumeanza kupata sura ya vazi la Taifa ili wadau
walijadili na waamue ni vazi gani la Mtanzania ambalo litawakilisha
Taifa kama nchi nyingine walivyomudu kuwa na vazi la Taifa.”
Aliongeza kuwa ili kufikia azma Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezoiandae tamasha maalumu kwa ajili ya kuonesha aina tofauti za nguo ili kupata vazi la Taifa.
Kadhalika,
Waziri Mkuu aliwaagiza waandaaji wa tamasha la Uridhi Festival
wahakikishe kuanzia mwakani kuwe na uratibu wa pamoja baina ya Tanzania
Zanzibar na Tanzania Bara ili tamasha lifunguliwe upande mmoja na
kufungwa upande mwingine wa Muungano.
Amesema
kwa kufanya hivyo watakuwa wametoa fursa kwa walio Zanzibar kujifunza
na kuona utamaduni wa bara na wa bara kujifunza ya Zanzibar, hivyo
itasaidia kudumisha umoja wa kitaifa. “Hakikisheni ikiwa tamasha
litafunguliwa Tanzania Bara basi lifungwe Zanzibar ili liweze kuwa na
tija’’.
Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, inaitaka Serikali kuongeza msukumo katika kukuza utalii na kutangaza vivutio vyetu vya utalii vikiwemo utamaduni na malikale.
“Mtakubaliana
nami kwamba tunapaswa kuendeleza mila, tamaduni na desturi zetu kwani
ndizo kichocheo muhimu cha uzalendo tulionao hususan katika suala zima
la maadili. Vilevile, utamaduni ni zao la uhakika kwenye sekta ya utalii
na ukarimu.”
Amesema
thamani ya utamaduni mara nyingi imekuwa ikionekana kwenye sekta
nyingine kama elimu, afya, michezo, kilimo, viwanda na maendeleo ya
jamii, ambapo alitoa rai kwaWizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
wadau wote wa utalii hususani Sekta binafsi na wananchi kwa ujumla
washirikiane katika kulinda, kutunza, kutangaza na kuendeleza vivutio
vya utalii nchini.
“Lengo
la Serikali ni kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,102,026 mwaka 2015
hadi 2,000,000 ifikapo mwaka 2020. Lengo hili linatekelezwa kwa
kuwezesha sekta binafsi kuwekeza kwenye huduma ya miundombinu ya utalii
na kuendelea kutangaza utalii ili kuwafikia watalii wengi zaidi.”
Amesema Urithi
Festival ni chachu ya kukuza, kulinda, kuimarisha nakutangaza utamaduni
na malikale zetu na kuvigeuza kuwa zao la utalii. Tamasha hili
litatuweka pamoja zaidi na kudumisha umoja, utaifa na uzalendo kwa nchi
yetu.
Aidha,
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuikumbusha Wizara ya Maliasili na
Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na
Mkoa wa Dodoma kuanza maandalizi mara moja ya kutekeleza agizo la
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan la kutenga eneo mahususi ambalo
litatumika kwa ajili ya Tamasha la Urithi kila mwaka kitaifa Mkoani
Dodoma.
“Napenda
kutumia fursa hii na hasa nikizingatia maagizo ya Makamu wa Rais kuwapa
changamoto Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wa utalii kuhakikisha
kuwa kuanzia mwaka kesho (2019) tamasha hili linatambulika Kimataifa na
kuwa moja ya kichocheo kikuu cha kukuza pato la Taifa litokanalo na
utalii“
Amesema
wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo Septemba 15, 2018 jijini Dodoma,
Makamu wa Rais, Mama Samia aliagiza kila Mkoa kutenga bajeti kwa ajili
ya Tamasha la Urithi. “Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha tena Wakuu wa Mikoa kuanza maandalizi mapema.“
“Tamasha
la Urithi sio tu linaenzi utamaduni na mila zetu, lakini ndio njia bora
zaidi ya kurithisha vizazi vijavyo mila, desturi, tamaduni na historia
yetu. Kwani yeyote yule ambaye haenzi utamaduni wake basi huyo ni
mtumwa.“
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 10, 2018.
No comments:
Post a Comment