NA MWANDISHI WETU, TABORA
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora Chiganga
Mashauri amesema kuwa waliokuwa viongozi wa chama Kikuu cha Wakulima
wa zao la Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) wanayo kesi ya
kujibu hivyo wanatakiwa kuleta utetezi wao.
Uamzi huo umetolewa leo na Hakimu Chiganga baada ya kusikiliza mashahidi
16 wa Jamuhuri katika shauri la Uhujumu Uchumi linalowakabili waliokuwa
viongozi wa WETCU.
Akisoma uamzi huo Hakimu Chiganga alisema ushahidi uliowasilishwa
na Jamuhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mwandamizi Shedrack
Kimaro umegusa mashitaka yote matano yanawakabili washitakiwa.
Watuhumiwa wa shauri hilo la kuhujumu uchumi namba 2/2017 ni Gabriel Mkandala,
John Kusaja, Prosper Mbacho, Hamza Kapera, Francis Penta, Msafiri Said na
mfanyabiashara Faras Yassin Abbas.
Mashitaka matano wanayotakiwa kujibu washitakiwa hao ni kula
njama, kughushi, matumizi mabaya ya ofisi, kufanya manunuzi bila kibali na kuisababishia
hasara Mamlaka ya serikali makosa ambayo inadaiwa waliyatenda kati ya Juni Mosi
hadi Julai 31/2015.
Shitaka la kwanza la kula njama ya kughushi nyaraka linawakabili Gabriel
Mkandala, John Kusanja, Msafiri Said na mfanyabiashara Faras Yassin
Abbas.
Shitaka la kughushi nyaraka linalowakabili Mkandala, Kusanja,
Mbacho, Kapera na mfanyabiashara Abbas inalodaiwa kuwa
walilitenda kati ya Tabora na Dar es salaam kwa kutengeneza Kadi ya
usajili wa gari namba T 181 VEN aina ya Toyota V8.
Shitaka la tatu la matumizi mabaya ya ofisi linawakabili Gabriel,
Kusanja, Mbacho, Kapera, Francis Penta, na Msafiri Said kuwa walinunua gari
namba T 181 VEN jambo ambalo lilisababisha hasara kwa chama hicho cha Ushirika.
Shitaka la nne dhidi ya watuhumiwa hao ni kwamba kwa makusudi na
huku wakijua kufanya hivyo ni kosa walinunua gari aina ya Toyota Land Cruser
V8 bila ya kupata kibali kutoka kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini.
Ilidaiwa katika shitaka la tano kwa watuhumiwa wote saba ,kwa makusudi
walisababisha hasara ya milioni 109 Chama hicho kutokana na
kununua gari aina ya Toyota Landcruser V8.
Upande wa utetezi ukiwakilishwa na Mawakili Hassan Kilingo na Kanani Chombala
umesema kuwa utakuwa na mashahidi wasiopungua 25 pamoja na nyaraka mbali mbali
kutoka Mamlaka ya Mapato –TRA na Ofisi
za WETCU.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Novemba tano mwaka huu litakaopoanza kusikiliza
utetezi wa washitakiwa ambao wameomba kusiwe na hailisho tena.




No comments:
Post a Comment