WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema ushirikiano mzuri baina ya taasisi mbalimbali za dini nchini na
Serikali ni jambo la muhimu katika kuboresha na kuimarisha amani.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Oktoba 22, 2018) alipowasili jijini Mwanza akiwa
njiani kwenda mkoani Simiyu ambako kesho anatarajia kufungua maonesho ya
wajasiriamali.
Alipowasili
kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Waziri Mkuu amepokelewa na Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, John Mongella na viongozi mbalimbali wa mkoa huo
wakiwemo wa Serikali na wa dini mbalimbali.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inatambua mkakati wa viongozi wa dini wa kuunda
kamati za amani nchini ambapo walianzia kwenye ngazi ya mkoa na sasa
wamefikia katika kata.
“Viongozi
wa dini mnadhamana kubwa katika kulifanya Taifa liendelee kudumisha
amani, utulivu na mshikamano, hivyo ushirikiano wenu na Serikali ni
muhimu.”
Amesema
viongozi wa Serikali wakati wote wamekuwa tayari kufanyakazi na
viongozi pamoja na taasisi mbalimbali za dini, lengo ni kuimarisha amani
na utulivu uliopo nchini.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Mwanza inawajibu wa kuhakikisha kwamba maeneo ya mkoa huu yanaendelea
kuwa salama.
Pia, Waziri Mkuu amempongeza Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Bin Mussa Kabeke kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
“Nakupongeza
kaimu sheikh wa mkoa kwa kuteuliwa na ninakutakia kila la heri katika
kazi yako na kwamba dhamana yako kubwa ni kuwaunganisha waislamu na
waumini wa dini zote.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma
JUMATATU, OKTOBA 22, 2018.




No comments:
Post a Comment