Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Tullo Chambo, akizungumza na waandishi habari jijini Arusha kuhusu Mashindano Wazi ya Taifa ya mchezo wa riadha 'Ngorongoro National Open
Championship,' yatakayofanyika jijini Arusha.
NA MWANDISHI WETU
WASHINDI
wa Mashindano Wazi ya Taifa ya mchezo wa riadha 'Ngorongoro National Open
Championship,' wanatarajia kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, kama moja
ya zawadi ya wale watakaofanya vizuri Desemba 14 jijini Arusha.
Hayo
yalisemwa na Katibu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday,
wakati akizungumza na gazeti hili kuhusiana na mashindano hayo yaliyopangwa
kuanza jijini Arusha katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Gidabuday
alisema katika mashindano hayo washindi wa mbio hizo, mbali na zawadi
zilizopangwa wao watakwenda kutembelea mbuga hizo kama moja ya vivutio kutoka
kwa wadhamini wa mashindano hayo.
Alisema
kutokana na hilo wanariadha wanapaswa kuongeza bidii katika mazoezi ambayo
wanafanya kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.
"Tumefurahi
sana kupata udhamini kutoka Ngorongoro tuna imani mashindano yatafana,"
alisema Gidabuday.
Alisema
mashindano hayo ni muhimu kwa wanariadha kuonyesha viwango vyao, jambo litakaloiwezesha
Kamati ya Ufundi ya RT kuwa na ‘base’ ya wachezaji walioko kwenye viwango hivi
sasa.
Alisema
mwaka uliopita kutokana na kutekeleza kalenda ya RT, hawakuwa na mashindano ya
Taifa, hivyo wameona ni lazima mwaka huu vijana wakapata nafasi muhimu
kuonyesha viwango vyao jambo litakalosaidia kuchagua timu ya Taifa.
Alisema
kuwa, washindi watakaofanya vizuri zaidi watapata fursa ya kushiriki mashindano
mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Japan, kusaka viwango vya kufuzu
mashindano ya kimataifa ikiwamo World Championship na Olimpiki.
Awali,
RT ilipanga mashindano ya taifa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, Novemba 16 kabla ya kuahirishwa.
Gidabuday
aliitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni Mita 100, Relay 100x4, 200, 400,
Relay 400x4, 800, 1,500, 5,000 na Mita 10,000, na KM 10,Kuruka Juu, Kuruka
Chini, Miruko Mitatu, Kurusha Mkuki, Tufe na Kisahani kwa wanaume na wanawake.
Alisema
kutakuwa na zawadi kwa washindi, ambapo mshindi wa kwanza atapata Medali ya
Dhahabu na Sh. 150,000, wa pili Medali ya Fedha na Sh. 100,000, huku wa tatu
akiondoka na Medali ya Shaba na Sh. 50,000.
Aidha,
alitoa wito kwa wadau wengine kuzidi kuiunga mkono Riadha Tanzania kama ambavyo
wanavyofanya Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment