HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 04, 2019

WANARIADHA WA TANZANIA WATAMBULIKA KATIKA VIWANGO VYA KIMATAIFA 'IAAF LABELS'

 Ezekiel Ngimba.
 Failuna Abdi Matanga-Tanzania (kushoto).
 Gabriel Geay.
Sulle.
 
WANARIADHA wanne wa Tanzania, wamefanikiwa kutambulika katika viwango vya kimataifa 'IAAF Labels' vinavyotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), kutokana na kufanya vema katika mashindano mbalimbali mwaka 2018.

Wanariadha hao na Klabu wanazotoka kwenye mabano ni Agustino Sulle, Gabriel Geay, Failuna Matanga (Talent-Arusha), na Ezekiel Ngimba (JWTZ). 

Sulle ameingia katika ‘Lebel’ ya Dhahabu ‘IAAF Gold Label’ kwa Full Marathon na Half Marathon baada ya kufanya vema katika mbio za Toronto Marathon huko Canada Oktoba 21 mwaka jana akitumia saa 2:07.46 akishika nafasi ya pili.

Ikumbukwe muda huo aliouweka Sulle, ndio rekodi mpya Tanzania kwa upande wa Marathon, akivunja ile ya 2:08 iliyokuwa imewekwa na Nguli Juma Ikangaa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Gabriel Geay, Boston 10 Km huko Boston Marekani Juni 24 akitumia dakika 28:24 nafasi ya kwanza na kuingia katika Label ya Fedha ‘IAAF Silver Label’ kwa Km 10 na Half Marathon.

Mwanamke pekee, Failuna Matanga, Cape Town Marathon Afrika Kusini akitumia saa 2:30.00 nafasi ya pili Septemba 23 ameingia Label ya Dhahabu ‘IAAF Silver Label’ kwa Half Marathon na Full Marathon pia yuko ‘Silver Label’ katika Mita 5000 na 10,000 akishiriki michezo ya Jumuiya ya Madola, Gold Coast Australia.

Ezekiel Ngimba, Frankfurt Marathon Uholanzi Oktoba 28 akitumia saa 2:13.32 ameingia ‘Label’ ya Shaba ‘IAAF Bronze Label’.

Kutokana na mafanikio hayo, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), linapenda kuwapongeza na kuwataka kuongeza bidii zaidi mwaka huu wa 2019.

“Sisi kama shirikisho tunapenda kuwapongeza kwa mafanikio haya vijana wetu, walimu wao na klabu zao kwa ujumla, kwani tunaamini kwa kujituma na ushirikiano wa pamoja ndiko kumeleta mafanikio haya ya kujivunia kwao binafsi na Taifa kwa ujumla,” alisema Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday.

Gidabuday, aliwapongeza makocha wa wanariadha hao, Thomas Tlanka na Francis John kwa mafanikio hayo ya wachezaji wao na kuwataka kukaza buti zaidi mwaka huu ili wazidi kupandisha viwango vya wachezaji wao na kuibua na kuendeleza vipaji vingine pia.

“Lakini wakati tukiwapongeza hawa, hii ichukuliwe ni changamoto kwa makocha na wachezaji wengine nao kuongeza bidii katika mazoezi huku wakitanguliza nidhamu ya ndani na nje ya mchezo ili nao waweze kufikia viwango hivyo kwa mwaka huu,” alisisitiza Gidabuday na kuwatakia kila la heri katika mwaka mpya wa 2019 uwe na mafanikio makubwa.

No comments:

Post a Comment

Pages