NA WAMJW-SIMIYU
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
ameiagiza wakala wa ujenzi (TBA) kupeleka fedha za ujenzi zilizotolewa
na Serikali katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
kuhakikisha zinafika ndani ya wiki mbili.
Agizo
hilo limetolewa leo wakati alipotembelea ujenzi wa jengo la Uchunguzi
na jengo la Mama na Mtoto na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo huku
sababu kubwa inayopelekea kusuasua ikitajwa ni fedha kidogo
zilizopokelewa na wakala wa ujenzi wa mkoa wa Simiyu kiasi cha Shilingi
Milioni 430 wakati serikali imetoa Bilioni 1.064 kwa ajili ya ujenzi
huo.
“Ninawashngaa TBA kwanini wanakaa na fedha
wakati wanajua mradi wa ujenzi unaendelea huku, serikali imetoa Bilioni
1.064 ili zitumike katika ujenzi wa Hospitali hii lakini TBA wameleta
milioni 430 tu, hizo fedha zingine ziko wapi?”. Alihoji waziri Ummy.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Ummy ameahidi kushughulikia suala hilo na kuahidi
fedha hizo zitafika katika mradi huo ndani ya wiki mbili ili ziweze
kusaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa majengo hayo ambapo yanatarajiwa
kukabidhiwa na kuanza kutoa huduma kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Kwa
upande wake Injinia mkuu wa TBA anayesimamia ujenzi huo Bw. Likimaitare
Naunga amesema fedha zilizoletwa katika mradi huo hazitoshi na ndiyo
sababu kubwa inayochangia kusuasua kwa mradi huo huku akitaka wakala wa
ujenzi (TBA) kuhakikisha fedha hizo zinafika mapema ili zisaidie
kuongeza kasi ya mradi na kufikia lengo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka amemuahidi Waziri Ummy kuwa
atasimamia kwa karibu upatikanaji wa fedha hizo zilizopo TBA zinafika
katika mradi na kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa
ili huduma muhimu za kibingwa zianze kutolewa Hopitalini hapo.
Wakati
huo huo waziri Ummy ametembelea Hospitali teule ya Somanda iliyopo
wilayani Bariadi na kuonekana kutoridhishwa na huduma zinazotolewa
katika jengo la Mama na Mtoto ambapo alishuhudia huduma mbaya
zinazotolewa kwa akinamama wajawazito na watoto wachanga.
Pia
Waziri Ummy ameshangazwa baada ya kuona hakuna chumba cha kuhifadhia
watoto wenye uhitaji wa huduma maalum kama huduma za joto kwa watoto
waliozaliwa kabla ya muda (Njiti) na kuitaka Hospitali hiyo kuwa na
chumba hicho muhimu.
Aidha, Waziri Ummy
ameshangazwa na kutokuwepo kwa huduma za upasuaji katika jengo hilo huku
sababu ikitajwa kutokuwepo kwa Sinki, hali inayosababisha usumbufu
mkubwa kwa akinamama wajawazito wanaofika kupata huduma hospitalini
hapo.
Kufuatia hali hiyo waziri huyo ametoa
siku tatu kwa uongozi wa Hospitali hiyo chini ya Mganga Mkuu wa Mkoa
Dkt. Mageda Kihulya kuhakikisha wananunua sinki hilo na huduma za
upasuaji zianze kutolewa mara moja katika jengo hilo.
No comments:
Post a Comment