NA TIGANYA VINCENT
NAIBU Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Abdallah Ulega ameagiza Afisa Mifugo wa Manispaa ya Tabora Cornelius Masawe
achunguzwe na achukuliwe hatua baada ya kutuhimiwa na wafanyabiashara wa mifugo
wa Mnada wa Ipuli kuwanyanyasa ikiwemo kuwatoza malipo zaidi bila kuwapa
stakabadhi.
Alisema tuhuma hizo ni
nzito kwa kuwa zinaweza kusababisha Serikali kukosa mapato yake ikiwa
wafanyabaishara hao watakaa kupeleka mifugo mnadani.
Ulega alitoa kauli hiyo
jana wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa mifugo kuhusu kuondoa mvutano
ulikouwa umezuka katika Mnada wa Ipuli uliopo Manispaa ya Tabora kuhusu
utaratibu wa usafirishaji ng’ombe kutoka na kuingia.
Alisema kuwa ni vema
vyombo vinavyohusika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa
(TAKUKURU) na vyombo vingine kuchunguza tuhuma zilizotolewa na wafanyabiashara
hao wa mifugo dhidi ya Masawe za kutoza fedha za faini ya mifugo bila ya
kukatia stakanadhi au kutoa ambayo halingani na malipo yaliyotolewa.
Kufuatia tuhuma hizo
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliagiza Masawe akamatwe na Polisi kwa
ajili ya mahojiano na TAKUKURU , kwa kushirikiana na Polisi kwa kushirikiana na
vyombo vingine vya kiusalama.
Alisema wafugaji kama
makundi mengine Mkoani Tabora wana haki sawa na haipaswi kunyanyaswa na
ikitokea wamenyanyaswa ni vema wakatoa taarifa mapema ili hatua ziweze
kuchukuliwa.
Mwanri alisema tuhuma
zilizotolewa na wafanyabiashara hao ni nzito haiwezekani zikapuuziwa ni vema
hatua zikachukuliwa ili kubaini ukweli na ikibidi na hatua za kulifilisha
katika maamuzi zifanyike haraka.
Baadhi ya wafanyabishara
walisema Masawe wakati wa kuendesha operesheni amekuwa akiwakata na kuwapiga
watu wanaokutwa na ng’ombe katika maeneo ambayo hayakatazwi kisheria.
Walisema ameweka
migambo katika kila pande ya kuelekea Mnadani ili kuwavizia na anawakamata anawatoza
shilingi 50,000/- kila ng’ombe kwa madai kuwa wanapita njia zisizo rasmi.
Walisema Masawe alishawi kupokea shilingi 900,000/- lakini aliandika stakabadhi ya laki 5 tu.
Walisema amekuwa
akiendesha zoezi hilo wakati akijua njia za kupitishia mifugo kwenda Mnadani
zimevamiwa na watu mbalimbali na kujenga.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri huyo amsema kuwa utaratibu wa nyuma wa kupeleka mifugo katika
Mnada wa Ipuli uendelee kutumika wakati suluhusho la kudumu kuhusu kuendelea au
kuhamisha likifanyiwa kazi kutokana na eneo hilo kuwa katikati ya mji hivi sasa
likitafutwa na pande zote.
Aliwataka wafugaji
kuendelea kutii Sheria zilizopo za Manispaa wakati wanaendelea kulitafutia
ufumbuzi wa kudumu suala lao la kupitisha ng’ombe kutoka kwao kwenda mnadani.
Ulega alisema tatizo
kubwa lilisababisha mvutano huo ni makosa yaliyofanyika nyuma ya kushindwa
kulinda njia ya kusafirisha ng’ombe kutoka maeneo mbalimbali na kwenda katika
Mnada wa Ipulu na kusababisha watu kujenga.
No comments:
Post a Comment