Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri (katikati), akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) baada ya kusikiliza kero zao kuhusu mwajiri kushindwa kuwasilisha michango wanayokatwa katika mishahara yao kila mwezi. (Picha na Tiganya Vincent).
NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI mkoani Tabora imetoa muda wiki
mbili kwa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuhakikisha
wamelipa adhabu ya milioni 40
wanazodaiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada
ya kuchelewesha michango ya watumishi wao.
Kauli hiyo imetolewa jana katika Kijiji
cha Karangasi wilayani Uyui na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya
kutembelea Kampuni hiyo ili kutatua mgogoro uliokuwepo baina yao na wafanyakazi
kuhusu michango ya NSSF.
Alisema ndani ya kipindi hicho Kampuni
hiyo inatakiwa kushirikiana na NSSF, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF) na
Ofisi yake kuhakiki orodha ya watumishi wa kampuni hiyo ambao wanafanyakazi
mkoani Tabora ili kuwa na uhakika wa malipo ya NSSF yanayopaswa kulipwa kila
mwezi.
Mwanri alisema ndani ya kipindi hicho
Kampuni ya CCECC itakiwa kuandaa mikataba ya watumishi wao na kuwasilisha
makato na michango kwa ajili ya NSSF za watumishi wao wanayodaiwa na nakala ya
vibali vya watumishi wa nje wanaofanyakazi Mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema ni jukumu la
Kampuni zozote zinazotekeleza majukumu yake mkoani humo kuhakikisha
zinazingatia Sheria za Nchi ikiwemo ya kuwasilisha michango ya asilimia 10
anazokatwa mtumishi na asilimia 10 anayopaswa kumchangia na kulipa asilimia 1
kwa ajili ya WCF. Alisema nje ya hapo mwajiri huyo
atahesabika anavunja Sheria za Nchi.
Naye Meneja wa NSSF Mkoa wa Tabora Shimo
Mussa alisema Kampuni hiyo imekuwa ikitoa taarifa za uongozi na hivyo
kuwasababishia kupoteza rasilimali za Shirika ikiwemo matumizi ya muda na
mafuta kufuatilia michango ya watumishi.
Aliongeza kuwa wakati mwingine wamediriki
kujificha pindi wanapogundua kuwa watumishi wa NSSF wanakwenda kufuatilia
michango na stahili za watumishi.
Mussa alisema Kampuni hiyo ya CCECC
iliwasilisha orodha ya watumishi zaidi ya 530 lakini ambao michango yao
imefikishwa kwenye Shirika na tena kwa kuchelewa ni milioni 76 ambayo ni sawa
na wafanyakazi 126.
Alisema kwa takwimu hizo zaidi ya
wafanyakazi 400 hawajulikani walipo na michango yao bado hajapelekwa na
kuongeza kuwa ni jukumu la mwajiri yoyote anapokuwa amepunguza watumishi
kuandika barua NSSF.
Baadhi ya watumishi walidai wamefanyakazi
miezi zaidi ya minne lakini hawana mikataba ya kazi, michango yao ya NSSF
inakatwa lakini haiwasiliswi sehemu husika, hawalipwi masaa ya ziada ya kazi na
Mwajiri amekuwa akiwabagua wakati wa utoaji wa huduma matibabu.
Kampuni ya CCECC inakazi ya kukarabati
reli ya Kati kutoka Dar es salaam hadi Isaka mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment