Mwalimu Neema Sio wa Shule ya Msingi Yamay, Mbulu mkoani Manyara, akishiriki kwa vitendo mafunzo ya ‘Kids Athletics’ yaliyokuwa yakiendeshwa na Mkufunzi Charles Maguzu wilayani Mbulu, juzi. (Na Mpiga Picha Wetu).
SSGT Catherine Lange wa Jeshi la Magereza akijiandaa kurusha mkuki katika mashindano ya Majeshi (BAMMATA).
NA MWANDISHI WETU,
MANYARA
WALIMU wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara, wametakiwa kwenda
kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo ya ‘Kid’s Athletics’ wanayopewa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mbulu, Joseph Mandoo, wakati akifungua mafunzo hayo ya siku yaliyoendeshwa na
Mkufunzi Charles Maguzu, ambaye pia ni Ofisa Michezo Mkoa wa Manyara.
Maguzu ni zao la Kozi ya Kids Athletics iliyoendeshwa na
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), chini ya Mkufunzi anayetambuliwa na
Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), Dk. Hamad Ndee.
Mandoo, aliwasisitiza walimu hao wakimaliza mafunzo hayo,
wakawafundishe wanafunzi wasiopungua 350 kila mmoja ili kuweza kuinua vipaji vyao
na kupunguza au kuondoa kabisa utoro shuleni.
Kwa upande wake Mkufunzi Maguzu, alisema hadi sasa amefundisha
jumla ya Walimu 716 katika Halmashauri mbalimbali nchini tangu ahitimu mafunzo
hayo.
“Hadi sasa nimefundisha jumla ya Walimu 716 katika
Halmashauri mbalimbali nchini, hivyo kila mmoja akifundisha Wanafunzi 350,
idadi ya Wanafunzi watakaokuwa wamefundishwa Kid's Athletics ni 250,600 hivyo
ni jambo la kushukuru,” alisema Maguzu na kuongeza.
Lengo langu ni kufikisha kwanza mafunzo haya kwa Walimu
1,000, hivyo naomba Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wadau na wadhamini
mbalimbali wazidi kuniunga mkono ili kuendelea kutoa utaalamu kwa walimu, ambao
ndio chachu ya kuibua na kuendeleza vipaji mbalimbali vya michezo kwa watoto.
No comments:
Post a Comment