Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)
akifungua kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi
kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Baadhi ya washiriki wa kikao kuhusu
ujumuishwaji wa masuala ya Kijinsia mahali pa kazi kutoka katika Wizara na
Taasisi za serikali wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo
pichani) wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Glonency Hotel,
mjini Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi Idara wa Utawala,
Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta akitoa neno la shukrani katika kikao
kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika kwenye
ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Picha ya pamoja.
Morogoro, Tanzania
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) amewataka waajiri serikalini kuzingatia kigezo cha ubunifu
wanapotekeleza zoezi la ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi ili
kuleta matokeo chanya na yenye tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila
siku.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa (Mb) amesema hayo mapema leo, alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku
mbili kinachohusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahala pa kazi
kilichofanyika mjini Morogoro.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa amesema kuwa, endapo waajiri watazingatia kigezo cha ubunifu na
kuacha kufanya kazi kwa mazoea serikali itapata watendaji kazi bora watakaoleta
matokeo chanya katika maendeleo ya nchi kwani watafanya kazi kwa uadilifu na
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi.
Mhe. Dkt.
Mwanjelwa (Mb) ameongeza kuwa, ubunifu katika utendaji kazi utawezesha
watumishi kuondokana na mitazamo hasi juu ya dhana ya jinsia ya kike kutegemea
kupata kazi kutokana na jinsi yao badala yake watambue kuwa vigezo na sifa za
kiushindani ndiyo vinazingatiwa.
“Tunapodai haki
zetu kama wanawake tuwe na hoja zenye mashiko zitakazoendana na sifa na vigezo
husika, tusiseme kuwa sisi ni wanawake hivyo tupewe nafasi” amesema Dkt.
Mwanjelwa.
Dkt. Mwanjelwa
amewataka waajiri kuzingatia vigezo vya ubunifu wanapoajiri wanawake na kutenga
bajeti kwa ajili ya ujumuishwaji wa masuala ya jinsia mahala pa kazi ili
kuboresha utendaji kazi.
Aidha, Dkt.
Mwanjelwa amewaagiza watendaji katika Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kuwa
kioo katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia mahala pa kazi ili kuepuka
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, rushwa ya ngono, ubaguzi wa aina yoyote,
upendeleo, ubadhilifu wa mali za umma na uvujishaji wa siri za serikali.
Naye,
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais , Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agnes Meena amesema kuwa, ofisi yake kama
mratibu wa masuala ya anuai za jamii imeona umuhimu wa kuandaa kikao cha
ujumuishaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kwa kushirikiana na
wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi Rasilimaliwatu kwa kuwa wao ndio
wahusika katika usimamizi wa mipango ya rasilimaliwatu na masuala yote ya kiutumishi.
Bi. Meena
amesema kuwa, kikao hicho kimefanyika kutokana na kuwapo kwa mwitikio wa
wastani katika utekelezaji wa masuala ya jinsia sehemu za kazi unaosababishwa
na kukosekana kwa utayari wa taasisi , mipango katika taasisi, mitazamo hasi,
unyanyapaa na ufinyu wa bajeji.
Akizungumza kwa
niaba ya washiriki wa kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala,
Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta amekiri kuwapo kwa changamoto katika
utekelezaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi na kuahidi kuwa kikao hicho
kitatoa maazimio yatakayoiwezesha serikali kutekeleza masuala ya kijinsia
ipasavyo mahali pa kazi.
Lengo la kikao
hicho ni kujadili fursa za masuala ya kijinsia katika utumishi wa umma na
kuweka mikakati itakayofanikisha Usawa wa Jinsia kwa Maendeleo Endelevu.
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 20 MACHI, 2019
No comments:
Post a Comment