HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 22, 2019

KIWANDA CHA TUMBAKU MBIONI KUJENGWA URAMBO

NA TIGANYA VINCENT
VYAMA Vikuu   vinavyolima  zao  la  Tumbaku Nchini (TCJE) vimeazimua kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Tumbaku mkoani Tabora .
Lengo la vyama hivyo ni kupata kiasi cha shilingi milioni 700 hadi mwisho wa msimu wa kilimo cha tumbaku mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini Tabora na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Wakulima wa Taumbaku hapa nchini Emanuel Charahani wakati wa mkutano wa 26 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU).
Alisema kuwa wazo la kiwanda hicho limeshajadiliwa na wajumbe wa vyama vyote ikiwemo cha Kigoma, Kahama na Mpanda na kuafikiwa sasa kilichobaki ni utekelezaji tu.
Charahani alisema wajumbe wa  Mkutano Mkuu wa WETCU kwa kauli mmoja wameazimia kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata zao la tumbaku wilayani Urambo mkoani Tabora.
Alisema kiwanda hicho kitasaidia sana kuhamasisha kilimo bora cha tumbaku na kuongeza uzalishaji maradufu tofauti na hali ilivyo sasa. 
Charahani alisema hakika vyama hivyo  wamedhamiria kujenga kiwanda hicho  ambacho kitaondoa urasimu wa makisio na kuongeza tija katika uzalishaji wa Tumbaku na  zaidi ya ajira  3000 zipatikana kila msimu wa kilimo cha Tumbaku .
Alisema ili kufanikisha ujenzi huo alishauri Wenyeviti na Mameneja wa vyama vikuu vya ushirika, Wenyeviti na Wakurugenzi wa halmashauri zinazolima zao la  tumbaku, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa na Mrajisi wa Mkoa wakutane Aprili 15, 2019 katika Ofisi za Bodi ya Tumbaku Tanzania ili kuunda kamati ya utekelezaji. 
Charahani alishauri kuanza mara moja kwa mchakato na upembuzi yakinifu huku akiutaka uongozi wa WETCU kusimamia ipasavyo zoezi hilo ili kuharakisha ujenzi.
Alisema kwamba hizo ni juhudi za wakulima kuhakikisha wanaungana  wadau kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya Tano dhidi ya viwanda.
Kwa upande wa  Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Uyui Said Ntahondi alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unasubiriwa kwa hamu kubwa na wakulima wa tumbaku hapa nchini kutokana na umuhimu wake.
Alisema wazo la ujenzi wa kiwanda hicho limepata baraka za vyama vyote vikuu vya ushirika wa wakulima wa zao hilo katika mikoa yote na kila mkulima amekubali kuchangia sh 9 kwa kila kilo atakazouza ili kufanikisha ujenzi huo.
Ntahondi alisema kwa kuchangia kiasi hicho katika msimu huu pekee wanatarajia  kukusanya zaidi ya sh milioni 700 kwa ajili ya kazi hiyo ambapo kinatarajiwa kujengwa kule Urambo ndani ya mkoa huo na eneo tayari limeshapatikana.
Alisisitiza kuwa kiwanda hicho ni mwarobaini wa kero ya muda mrefu ya mkulima kuwekewa ukomo wa kilo za kuzalisha wakati ana uwezo wa kuzalisha zaidi ya kiwango hicho. 
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Collins Nyakunga aliutaka uongozi wa Halmashahuri ya wilaya ya Urambo kukaa meza moja na Vyama Vikuu vya Ushirika vya Milambo na WETCU kabla ya kuanza ujenzi huo ili kuepusha migongano ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

Pages