HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 06, 2019

RT, NCAA wasaini makubaliano maalum ya udhamini

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  (NCAA), Dk. Fred Manongi, akisaini makubaliano maalum (MOU), na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kusapoti programu mbali mbali za mchezo wa riadha kuelekea Michezo ya Olimpiki Tokyo Japan 2020. Wanaoshuhudia kushoto ni Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday na Mjumbe Kamati Tendaji ya RT, Meta Petro.  (Picha na Tullo Chambo).
 


NA MWANDISHI WETU 

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limeingia makubaliano maalum na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambako mamlaka hiyo imetoa udhamini mnono kuelekea Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika, Olimpiki ya Tokyo, ikiwa ni pamoja na kudhamini Ngorongoro Race kila mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, kupitia makubaliano hayo, RT limepata udhamini mnono kuelekea Mashindano ya Dunia ya Nyika hadi Olimpiki ya Majira ya Joto mwaka 2020, yatakayofanyika Tokyo, nchini Japan.

Alibainisha kuwa, RT na Mamlaka hiyo pia wameimeingia makubaliano rasmi ya kudhamini mashindano ya Ngorongoro Race, yanayofanyika Aprili kila mwaka mjini Karatu.

“Haya ni makubaliano mapya baina yetu, lakini ikumbukwe kwamba RT tayari ilishaanza kufanya kazi kwa pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenye matukio zaidi ya matatu yanayohusu mchezo wa riadha,” alisema Gidabuday na kuyataja maeneo hayo kuwa ni;

Mbio za Nagai Marathon zilizofanyika Japan Oktoba mwaka jana, Mashindano ya Taifa yaliyofanyika Desemba 14, 2018 jijini Arusha, pamoja na Mashindano ya Taifa ya Mbio za Nyika, yaliyokimbiwa Februari 16, mwaka huu mjini Moshi.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo (MoU) katika Ofisi Kuu ya Mamlaka, ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Mhifadhi Mkuu Dk. Fredy Manongi, aliwataka wanariadha kuleta ushindi ili kulitangaza vyema jina la Tanzania na vivutio vyake nje ya mipaka.

Aidha, Manongi alisema wamefikia hatua yaa kuingia makubaliano na RT ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla, kutumia michezo kutangaza Vivutio vya Maliasili na Utalii.

Kwa upande wake, Gidabuday, ambaye aliambatana na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya RT (Meta Petro na Tullo Chambo), baada ya kusaini kwa niaba shirikiaho lake, aliahidi kwamba mkataba huu utatendewa haki kwa malipo yote kuidhinishwa kwa kutekeleza madhumuni yaliyokuwemo kwenye maudhui ya andiko la kuomba fedha hizo ambazo ni;

Maandalizi ya Kambi za Taifa kuelekea mashindano ya (Mbio za Nyika za Dunia, Mashindano ya All African Games, Mashindano ya Dunia mjini Doha, Qatar na Olimpiki ya 2020 Tokyo.

Aidha, historia hiyo ilikamilishwa na kusainiwa kwa mkataba mwingine muhimu mbele ya Katibu Mkuu wa RT, kati ya Meta Sports Promotion ambao ni waandaaji wa Ngorongoro Race na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo kwa mwaka huu yatafanyika April 20, 2019 mjini Karatu.

Mashindano hayo mwaka huu yataanzia lango la geti ya Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu.

Gidabudai amewapongeza Meta Sports Promotion kwa kuweza kuendesha mbio hizo za Ngorongoro Race kwa miaka 13 sasa ambapo mwaka jana mgeni rasmi alikuwa Mhe. Dk. Kigwangalla, ambaye alitoa agizo la kutumia Michezo kutangaza Vivutio vya Utalii na Maliasili za Utalii wa Nchi yetu.

Aliwaasa familia ya wanariadha kuiga mfano wa wa Meta Sports Promotion katika kuendeleza maendeleo ya mchezo wa Riadha Tanzania badala ya kuendelea kulalamika bila vitendo.

No comments:

Post a Comment

Pages