NA JOHN MARWA
WAKATI
wadau na mashabiki mbalimbali wa soka wakimpigania Beki wa Simba,
Shomari Kapombe, kunufaika na zawadi zinazotolewa baada ya Timu ya Taifa
‘Taifa Stars’ kufuzu Fainali za Afrika (AFCON), Nahodha Mbwana Samata,
naye amekazia.
Baada
ya Stars kufuzu kwa kuwafunga Uganda ‘The Cranes’ Jumapili iliyopita
mabao 3-0, juzi Rais Dk. John Magufuli, aliwaalika Ikulu jijini Dar es
Salaam kula nao chakula cha mchana na kisha kuwapa zawadi ya viwanja
jijini Dar es Salaam.
Mara
baada ya tukio hilo, wadau na mashabiki mbalimbali walianza kutoa maoni
yao ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii, wakitaka TFF waangalie pia
nyota waliotoa mchango wao katika safari ya Stars kufuzu, huku wakimtaja
Kapombe aliyeumia akiwa na timu hiyo kambini Afrika Kusini wakati
ikijiandaa kuivaa Lesotho.
Awali
kuelekea mechi ya Uganda, pia Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Stars
Ishinde, Paul Makonda, alitoa ahadi ya Sh. Milioni 10 kwa kila mchezaji
endapo watafanikiwa kufuzu.
Samata,
aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter, akiiomba TFF kumjumuisha beki
huyo katika zawadi zilizotolewa, kwani anaamini kama Kapombe angekuwa
yupo fiti angekuwepo sehemu ya kikosi kilicholiletea Taifa heshima
kubwa.
Amesema
kama TFF watashindwa kufanya hivyo, anawaomba wachezaji wenzake
kumchangia kidogo kidogo na endapo itashindikana, basi binafsi atagawana
naye nusu kwa nusu ahadi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Stars
Ishinde, Paul Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kama
Captain ningeomba TFF imuangalie Shomari Kapombe katika zawadi ambazo
wachezaji watapata, ikishindikana basi ningeomba wachezaji wote
tumchangie kidogo kidogo na endapo vyote visipowezekana kabisa, basi
katika ahadi ya Mh. Paul Makonda, nitagawana nae nusu kwa nusu,”
ameandika Samata.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa kamati hiyo, hakubainisha ahadi itatekelezwa lini.
No comments:
Post a Comment