Baadhi ya Makatibu Tawala wa Mikoa nchini na wafanyakazi wa Wizara ya
Maji waliohudhuria katika mkutano huo.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali
kupitia wizara ya maji imejipanga kuleta utaratibu wa kuziwekea mikataba ya utendaji
kazi taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya
maji katika ngazi mbalimbali nchini.
Hayo
yamezungumzwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa wakati
alipokuwa akifungua mkutano uliowahusisha Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kwa ajili ya kujengeana
uelewa wa pamoja kuhusu uendeshaji mpya wa sekta ya maji kufuatia kupitishwa
kwa sheria mpya ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Sheria Namba 5 ya mwaka
2019.
Prof.
Mbarawa amesema kuwa wizara imeamua kuja na mikataba hiyo itakayokuwa na
malengo maalum ya kuzipima taasisi kwa kila mwaka mmoja ambapo nia ya serikali
sio kumkomoa mtendaji bali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma
iliyokusudiwa.
“Mamlaka
hizi zikisimamiwa kwa malengo zitafanya kazi vizuri zaidi na zitakuwa na uwezo
mkubwa wa kujiendesha pia kupimana utendaji kazi ni jambo zuri kwa sababu
tukifanya kazi kimazoea mamlaka na taasisi zetu hazitoweza kufanya kazi vizuri
wala kuimarisha utoaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi wetu,” amesema
Prof. Mbarawa.
Ameendelea
kusema kuwa, mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais
Magufuli alilolitoa mwezi Mei, 2018 kuhusu mfumo wa uendeshaji wa sekta ya maji
ambapo aliagiza sekta ya maji isimamiwe na wizara moja ili kurahisisha
usimamizi na uwajibikaji wa watendaji.
Nae
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Kitila Mkumbo amefafanua kuwa Sheria ya
Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Namba 12 ya mwaka 2009 imepitiwa na
kutungwa upya na kwa sasa inajulikana kama Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa
Mazingira ya mwaka 2019 ambapo kikubwa katika sheria hiyo ni kuanzishwa kwa
Wakala wa Maji Vijijini.
“Haitawezekana
kukamilisha mipango ya sekta ya maji bila ushirikiano wa kutosha kutoka kwa
Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo kupitia mkutano huu Makatibu Tawala watapata
nafasi ya kupitia na kuielewa sheria mpya kwa kina na kubaini nafasi zao katika
usimamizi na uendeshaji wa sekta ya maji kwenye sheria hii," amesema Prof.
Mkumbo.
Kuanza
kutumika kwa sheria hiyo mpya kutaimarisha mfumo wa utoaji huduma za maji na usafi
wa mazingira nchini, kutaongeza ufanisi na uwajibikaji katika kutoa huduma za
maji, kutaimarisha ujenzi na usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji, kutachochea
utendaji katika sekta nyingine na
kuongeza mchango wa sekta ya maji katika uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment