TIMU ya Taifa ya Mbio
za Nyika inatarajiwa kuagwa rasmi kesho Machi 27 jijini Dar es Salaam tayari kwa safari ya
kwenda mjini Aarhs Denmark katika mashindano ya Dunia 'IAAF World Cross Country' yatakayorindima Machi 30
mwaka huu.
Timu hiyo ya Taifa ambayo
ilikuwa kambini jijini Arusha kwa takribani mwezi mmoja chini ya ufadhili wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), na DStv, iliwasili jijini Dar es
Salaam jana tayari kwa safari leo usiku.
Kwa mujibu wa Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, timu iko katika
hali nzuri na vijana wana ari ya kwenda kupeperusha vena Bendera ya Taifa huko
Denmark.
Gidabuday, alisema
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe,
ataongoza hafla ya kuipa Baraka za mwisho timu hiyo ikiwamo kukabidhi Bendera
ya Taifa, akiungana na viongozi mbalimbali kuanzia saa 8 mchana kwenye ukumbi
wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katibu huyo, alisema
katika hafla hiyo pia wamemualika Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis
Kigwangalla, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka ya Ngorongoro, Mkurugenzi wa Multchoice Tanzania na Kurugenzi za
Michezo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Msafara wa timu hiyo
ya Tanzania unaundwa na watu 20, wachezaji 16 na viongozi wanne.
Aliwataja viongozi
hao ni Makamu wa Pili wa Rais- Ufundi RT, Dk. Hamad Ndee ambaye ni Mkuu wa
Msafara, Kocha Mkuu Meta Petro, Kocha Msaidizi Madai Jambau na Matron Marcelina
Gwandu.
Wachezaji kwa upande
wa wanaume ni Marko Monko, Joseph Panga ‘Mti Mkavu’, Faraja Damas, Emmanuel
Giniki, Gabriel Geay, Francis Damiano na Yohana Elisante.
Wanawake ni Failuna Matanga,
Magdalena Shauri, Angelina Tsere, Sisilia Ginoka, Mayselina Mbua, Amina Mgoo, Anastazia
Dolomongo, Aisha Magelani na Natalia Elisante.
Timu hiyo itaondoka usiku wa Machi 27 kwa ndege ya KLM na inatarajiwa kurejea nchini Machi 31.
No comments:
Post a Comment