Kaimu Naibu Mrajisi Udhibiti wa Tume ya
Maendeleo ya Ushirika Collins Nyakunga akitoa mada jana kwenye mkutano wa
26 Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU)
ulifanyika mjini Tabora.
Tume ya Maendeleo ya
Ushirika imewaonya watendaji na viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini kuacha
tabia ya utoaji wa posho kwa wajumbe wake kipindi cha uwasilishaji wa taarifa
ya mapato na matumizi ili kuwafanya waache kusikiliza kinachowasilishwa.
Kauli hiyo imetolewa
jana mjini Tabora na Kaimu Naibu Mrajis Udhibiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Collins
Nyakunga wakati wa Mkutano wa 26 wa Chama Kikuu
cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU).
Alisema baadhi ya
viongozi na watendaji wamekuwa wakitumia kipindi ambacho taarifa ya mapato na
matumizi inawasilisha kulipa posho kwa wajumbe ili kuwafanya wasisikilize kwa
umakini na hatimaye wasiwe na muda wa kuhoji sehemu zenye mapungufu na dosari.
Nyakunga alisema utoaji
wa posho za wajumbe na wageni waalikwa hazipaswi kuingilia na uwasilishaji wa
taarifa zozote kwa kuwa kufanya hivyo kunaonyesha viongozi na watendaji kuna
kitu wanaficha.
Aidha aliwataka
wajumbe wanapokuwa kwenye Mkutano ni vema wakasikiliza kwa makini na pindi
wanapoona sehemu kuna mapungufu wawe huru kuhoji kwa ajili ya kuujenga ushirika
ulio imara badala ya kuacha mapungufu yaendelee bila kuchukua hatua hali
inayoweza kuudhofisha ushirika wao.
Akisoma hotuba ya
mgeni rasmi, Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Tabora Raphael Nyanda alivitaka
vyama vyote vya Ushirika kuhakikisha vinafunga vitabu vya hesabu ndani ya miezi
mitatu baada yam waka wa fedha kuisha na kuviwasilisha kwa Mkaguzi wa Nje.
Alisema baada ya
ukaguzi matokeo yake yasomwe katika Mkutano Mkuu wa Ushirika ili wajumbe
wafahamu mwenendo mzima wa Ushirika kwa ajili ya kuchukua hatua kama wanaona
viongozi wao wanawapeleka pabaya.
No comments:
Post a Comment