NA TIGANYA VINCENT
SERIKALI ya Mkoa wa
Tabora imewaonya wanachama wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda
ya Magharibi (WETCU) kutochangua viongozi wenye historia wizi , ubadhilifu na
wenye matendo ambayo ni kinyume cha Sheria za Nchi kwa kuwa haitasita kuwaondoa
kama watawachagua.
Kauli hiyo imetolewa
jana mjini Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri katika hotuba yake
iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi Raphael Nyanda wakati wa Mkutano wa 26 wa
WETCU ambao pamoja na ajenda nyingine ni uchaguzi wa viongozi.
Alisema viongozi wanaotakiwa
ni wale waadilifu na waaminifu na wenye maono ya kuwaletea wanachama maendeleo
na kuweka maslahi ya wanachama mbele badala ya kufikiria maslahi binafsi ili
kuinua ushirika nchini.
Mwanri alisema baadhi
ya wanachama wanaomba kuchaguliwa kwa ajili ya maslahi binafsi na kutaka kugeuza
Ushirika kuwa maficho ya kuwanyonya wakulima na kuwafanya washindwe kuendelea.
“Mwanachama wa
ushirika anayetaka kugombea lazima ajipime kama yuko safi na
mwadilifu na sio kibaka mzoefu ndio aombe kuchaguliwa kuwaongoza
wenzake” alisema.
Mwanri aliwataka
wanachama kuwaondoa mara moja watu wanaofanya ujanja ujanja kwa ajili ya kutaka
kujiingiza katika uongozi wa ushirika kwa nia ya kuwanyonya wakulima kabla mambo
hajaharibika.
Naye Kaimu Naibu
Mrajis Udhibiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Collins Nyakunga alisema kuwa endapo
wanachama watafanya makosa ya kuchagua viongozi wowote kwa ushawishi wa fedha ,
Ofisi ya Mrajis haitasita kuwaondoa.
Aliongeza kiongozi
atakayebainika kuingia madarakani kwa kutumia fedha ataondolewa madarakani hata
kama ameshachaguliwa na hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nyakunga alisema mtu
anayetafuta uongozi katika Ushirika lazima awe ni yule ambaye yuko tayari
kuwasidia wanaushirika kusonga mbele na kujiletea maendeleo na sio
kuwadidimiza.
No comments:
Post a Comment