WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefungua mradi wa ujenzi na ukarabati mkubwa wa
kituo cha afya cha kata ya Koromije wilayani Misungwi na amewahakikishia
wananchi kuwa Serikali imejipanga vizuri kuboresha huduma za afya.
Amesema
uboreshaji huo unahusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara,
chumba cha kujifungulia, wodi ya mama na mtoto na wodi ya wanawake na
wanaume pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.Uboreshaji huo unagharimu sh. milioni 500.
Waziri
Mkuu alifungua mradi huo jana (Jumanne, Machi 19, 2019) akiwa ziarani
Misungwi, ambapo aliwataka wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali
yao, ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.
“Hapa
zamani kulikuwa na zahanati yenye jengo moja, tumeamua kuboresha na
kupandisha hadhi na kuwa kituo cha afya. Rais Dkt. John Magufuli anataka
wananchi wapatiwe huduma muhimu zikiwemo za afya karibu na makazi yao”.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu alisema hakuna kijiji chochote nchini kitakachoachwa bila
ya kuunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini
(REA), vikiwemo na vya wilaya ya Misungwi tena kwa gharama nafuu.
“Rais
wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga
fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote
vikiwemo na wilaya yenu hii ya Misungwi. Gharama za kuunganishiwa umeme
huo ni sh. 27,000 tu.”
Waziri
Mkuu aliongeza kwamba lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye
vijiji vyote Tanzania na vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na
gridi ya taifa vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira
na kukuza uchumi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 19, 2019.
No comments:
Post a Comment