Na Mwandishi Wetu
Dar es
Salaam. Jumla ya klabu 10 zimethibitisha kushindana katika mashindano ya klabu
bingwa ya mchezo wa kuogelea yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la
Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Upanga jijini Dar es Salaam.
Mashindano
hayo yamepangwa kufanyika Aprili 13 na 14 na yamedhaminiwa na kampuni za Asas,
Samsung, DTB Bank, Snow Cream, Knight Support na kituo cha utangazaji cha
Clouds FM.
Mwenyekiti
wa Kamati ya maandalizi wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Hadija Shebe
amezitaja klabu hiyo kuwa ni Bluefins, Champion Rise, Mis Piranhas, klabu ya
kuogelea ya Mwanza (MSC), FK Blue na Wahoo ya Zanzibar.
Hadija
amezitaja klabu nyingine kuwa ni ISM-Moshi, ISM-Arusha,FK Blue Marlins,
Talis-IST na mabingwa watetezi, Dar es Salaam Swim Club (DSC).
Alisema kuwa
mashindano hayo yamepangwa kuanza saa 2.00 asubuhi siku ya Jumamosi na
waogeleaji watashindana katika staili tano ambazo ni Freestyle, Breaststroke, Butterfly, Backstroke na Individual Medley.
Kwa mujibu
wa Hadija, waogeleaji hao pia watashindana katika relay katika mashindano
ambayo yamepitishwa na Shirikisho la Mchezo wa kuogelea Duniani (Fina) kuwa ya
kutafuta alama za kufuzu mashindano ya Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini
Korea mwezi Julai.
“Tunatarajia
kuona ushindania mkali kwa waogeleaji
wetu ili kutafuta nafasi ya kufuzu mashindano ya dunia. Waogeleaji wengi wapo
katika maandalizi ya mwisho mwisho kwa ajili ya mashindano hayo, bado
tunahitaji wadhamini wa mashindano haya,” alisema Hadija.
Kwa mujibu
wa Hadija, kutakuwa na jumla ya vipengele
vya mashindano 108 na kila klabu imetakiwa kuwakilishwa na waogeleaji
wawili katika kila kipengele cha mashindano ambavyo pia vimepangwa kutokana na
umri.
“Zaidi ya
waogeleaji 200 watashiriki katika mashindano haya makubwa ya Tanzania. Tunaomba
wadau wajitokeze kusaidia na kuwapa hamasa waogeleaji wetu ambao kwa sasa
wamepata mafanikio makubwa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,” alisema.
No comments:
Post a Comment