HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 12, 2019

KOPENI KWA MALENGO YA KUJIPATIA MAENDELE-DAS UYUI

Mkazi wa Kijiji cha Lutende wilayani Uyui, Issa Said Mtiliga akitoa neno la shukurani jana kwa wakufunzi kutoka Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kuwajengea uwezo wakulima 100 waliopimiwa mashamba yao na kupata hati miliki za kimila ili waweze kutumia mtaji huo kuboresha ufugaji wa mifugo ikiwemo kuku wa kienyeji.

NA TIGANYA VINCENT

SERIKALI ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora imewatahadharisha wakazi wa vijiji vya Miyenze na Lutende kutokopa fedha katika Taasisi za fedha bila malengo kwa ajili ya kuepuka kunyang’anywa ardhi zao baada ya kushindwa kulipa madeni.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Uyui Moses Pesha wakati wa kufunga mafunzo ya kujengewa uwezo wakulima 100 na viongozi 10 wa Kijiji cha Lutende na kukabidhiwa hati miliki za kimila.

Alisema Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania(MKURABITA) umeletea neema kwao ni vema wanapotaka kutumia hati zao kukopa iwe kwa kazi maalumu na sio kukopa kopa ovyo ovyo bila kuwa na mipango mizuri ya kutumia fedha watakazokopeshwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

“Hakikisheni mnapokopa iwe kwa ajili ya kazi maalumu na sio kwa ajili ya starehe , anasa na kununua mavazi na urembo…unapokopa hakikisha unalipa deni kwani usipolipa deni hati hizo zitakuwa sio za kwenu tena hivyo mashamba yenu yatachukuliwa na Taasisi zilizowakopesha” alisema.

Pesha alisema sio vizuri mmoja wa wanafamilia akafanya siri wakati wa kwenda kukopa huku wenzake hawajui, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha mgogoro baina yao na kufanya kuendelea kuisha kimasikini.

Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Wilaya ya Uyui amewaonya wakazi wa Vijiji hivyo waliopatiwa hati miliki za kimila baada ya ardhi kupimwa kuepuka kuuza ovyo maeneo yao kwa kuwa wanaweza kusababu kuwa na maskini na kurudisha migogoro.

Alisema mwananchi anapotaka kuuza ardhi ni vema awe na sababu ya msingi na pia katika kuuza lazima afuate taratibu na sharia zilizopo ili kuepuka kujiingiza katika umaskini.

Pesha aliongeza kuwa hata wanapouziana ni vema wafuate utaratibu wakati wa ubadilishani hati ili kuepuka migogoro baina ya mnununuzi na wanafamilia katika siku za baadae.

Naye Meneja Urasimishaji ardhi Vijijini kutoka Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania(MKURABITA) Antony Temu alisema mafunzo waliotoa kwa wakazi wa Kijiji cha Lutende na Miyenze katika Wilaya ya Uyui yamewajengea uwezo wakulima wote waliopata hati ili waweze kutumia mtaji huo kuboresha ufugaji wa mifugo ikiwemo kuku wa kienyeji.

Alisema pia wanapewa elimu ili waboreshe kilimo , utunzaji wa kumbukumbu za hesabu za kilimo na biashara na uandishi wa mpango wa biashara na uundaji wa vikundi vya uchumi kwa ajili ya uboreshaji wa uchumi wao na wilaya kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages