Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Athumani Kihamia
akizungumza an wafanyakazi wa NEC (hawapo pichani).
Mkurugenzi
wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu wa NEC, Gerald Mwanilwa akifafanua
jambo.
Baadhi ya wafanyakazi wa NEC wakimsikiliza
Dkt. Kihamia.
Baadhi ya wafanyakazi wa NEC wakimsikiliza
Dkt. Kihamia.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt.
Athumani Kihamia ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa tume
hiyo kutokana na kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano, weledi na uzalendo.
Dkt. Kihamia ameeleza hayo wakati alipokutana na wafanyakazi
wa NEC kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu
utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Alisema katika kipindi alichokaa Tume amegundua kuwa sasa utendaji
kazi wa mazeoa umepungua na watumishi wengi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao
kwa wakati, kwa uaminifu, kutunza siri na kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya
lazima.
Mkurugenzi huyo wa NEC alifafanua kuwa katika kikao chake cha
kwanza na watumishi wa Tume cha Agosti 7 mwaka 2018, alijadili changamoto
zinazowakabili watumishi hao ambazo zilikuwa kikwazo cha utekelezaji wa
majukumu yao kwa njia moja au nyingine.
“Tuligundua kuwa changamoto nyingi zilitokana na tabia binafsi
za baadhi ya watumishi, na baadhi yao kufanya kazi kwa kuigiza yaani kwa mazoea
kwa kisingizio cha mchakato”, alisema Dkt. Kihamia na kufafanua kuwa:
“Lakini sasa hivi jambo la kufurahisha asilimia kubwa ya
watumishi wanafanya kazi sio kwa mazoea, lakini pia ufanisi wa kazi zao
umeongezeka kwa kiwango kikubwa”.
Alibainisha kuwa kwa sasa Tume imeimarika vya kutosha kwa
kuwa wakati alipofika wastani wa utendaji kazi ulikuwa asilimia 52, ikimaanisha
kuwa zaidi ya asilimia 48 ya watumishi walikuwa hawawajibiki ipasavyo, lakini
sasa uwajibikaji umefikia wastani wa asilimia 65 baada ya kuwekeana malengo.
“Kwa hiyo tulipo sasa tupo juu ila ni lazima tuendelee kuwa
kitu kimoja, ingawa katika kuimarika
huko wapo wenzetu wachache sana wenye matatizo madogo madogo, hivyo wanatakiwa
warekebishwe” alisisitiza Dkt. Kihamia
Alifafanua kuwa kuimarika kwa utendaji kazi ni jambo kubwa
kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa kutowajibika ipasavyo kwa watumishi wa umma katika
nchi nyingi za Afrika kumesababisha udumavu wa maendeleo ya nchi hizo.
Hivyo aliwataka watumishi wa NEC kuendeleza tabia ya
uwajibikaji kwa mustakbali wa maendeleo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na
Tanzania kwa ujumla kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwa chachu ya
maendeleo ya nchi.
Ili kuboresha zaidi utendaji kazi wa Tume, Dkt. Kihamia aliziagiza
kila idara ziainishe vipaumbele (priorities) vitakavyotekelezwa na idara husika
kwa kipindi chote kuanzia Julai 1 mwaka huu.
Alisema baada ya kupata vipaumbele hivyo kutoka kila idara vitaunganishwa
kupata vipaumbele vya Tume na aliwataka watumishi kutambua kuwa majukumu ya
kila idara ni majukumu ya Tume hivyo ni muhimu kuwa kitu kimoja katika
kuyatekeleza.
“‘Checklist’ ni jambo kubwa sana kwa sababu kuna mtu ukienda
kwenye idara yake ukimuuliza amefanya mambo gani, anaweza akawa amefanya mambo
mazuri tu lakini hayakumbuki mpaka ayafikirie ndio akwambie” alisema Dkt.
Kihamia na kufafanua kuwa:
Alisema checklist ni mpango kazi ambao hata watafiti
wanaofanya tafiti za kisasa wamegundua kwamba kampuni nyingi za kibiashara
zinazofilisika ni zile ambazo hazina checklist za kisasa.
“Kwa hiyo checklist ni moja ya agenda ambayo nimekuja
kuizungumzia leo kwa sababu tunafanya kazi kwa mipangokazi na unapokuwa na
checklist unajua hili nimelifanya hili sijafanya” alisema Dkt. Kihamia.
Alisema mtumishi asipokuwa na checklist ya kazi zake hawezi
kuwa na muendelezo (consistency) mzuri wa majukumu ambayo mtumishi anataka kuyatekeleza
na ukamilifu wa kazi zake hautakuwepo.
Alisema wataalamu wanasema kwamba checklist ndio njia pekee
kwa sasa inayoaminika katika kutekeleza majukumu kwa ufasaha.
“Mtafiti mmoja aliwahi kusema checklist ni aina ya mpangilio
wa majukumu ambao unapunguza kushindwa (failure)katika kazi, ina maana
usipokuwa na checklist uwezekano wa kushindwa ni mkubwa” aliongeza Dkt.
Kihamia.
Kwa upande mwingine Dkt. Kihamia alimtaka kila mtumishi wa
Tume atambue majukumu ya msingi ya NEC na ikiwemo kufahamu Uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura ni nini na kufahamu taratibu zote za uchaguzi.
“Watu wajifunze kuwepo kwa nafasi wazi ni nini maana watu
wanalalamika kwamba Serikali inatumia fedha nyingi kufanya chaguzi ndogo za
mara kwa mara lakini wanasahau kwamba suala hilo lipo kwenye katiba na ni
utarabu.” alisema Dkt. Kihamia.
Dkt. Kihamia tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amejiwekea utaratibu wa kukutana na watumishi wa
tume hiyo huku hiki kikiwa ni kikao chake cha tatu.
Katika kikao cha kwanza cha tarehe 7 Agosti mwaka 2018, Dkt.
Kihamia aliainisha vipaumbele vyake 30 vya kuzingatia katika utekelezaji wa
majukumu ya Tume na kuvifanyia tathmini kwenye kikao cha pili kilichofanyika
mwezi Desemba mwaka 2018.
Baadhi ya vipaumbele alivyosisitiza ni kuweka mpango kazi wa
kila idara, kitengo na mtumishi na utekelezaji wake kwa kile mwezi, kuandaa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya
kila idara, kutambua madeni ya kila idara na kitengo na kuonesha kama
yamehakikiwa au la, sababu ya madeni hayo na kuwepo rejesta na mpango kazi wa
malipo.
Katika vikao hivyo wakuu wa Idara wamepewana nafasi ya
kufafanua mambo mbalimbali katika idara zao na watumishi kuwepo nafasi ya
kueleza mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
No comments:
Post a Comment