HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 20, 2019

SIMBA KUTAWAZWA MABINGWA NAMFUA!!

Kikosi cha Simba.


NA JOHN MARWA

HAKUNA namna watakiepuka kikombe cha dhahama!! Unaweza kusema maneno hayo ukiwa unasuburia kushuhudia dakika 90 za kishujaa kati ya Singida United dhidi ya Mfalme wa Nyika Simba SC.

Ni mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara TPL unaotarajiwa kuchukua nafasi kunako Uwanja wa Namfua mjini Singida, ukiwa na ukakasi kwa mwenyeji kujaribu kusaka ushindi kwa mnyama aliyejeruhiwa akihitaji walau pointi moja kujitangaza mwamba mtawalia kunako TPL msimu huu.

Simba wanateremka kwenye pambano hili wakihitaji ushindi kutawazwa mabingwa wapya wa TPL ama sare ambayo itawafanya kufikisha pointi 89 ambazo zitafikiwa na watani zao Yanga SC lakini wakiwa na jeuri ya mtaji wa mabao 74 ya kufunga na 14 ya kufungwa, faida ya mabao 60 kibindoni.

Yanga wako mabegani mwao wakiwa nafasi ya pili na pointi 83 za michezo 36, wakifunga mabao 55 na kuruhusu mabao 25, faida ya mabao 30, jambo linalowalizimu kuwaombea watani zao kupoteza michezo iliyosalia na wao kushinda yao miwili kwa idadi ya mabao si chini ya 15 kila mtanange.

Kama vijana wa Mbelgiji Patrick Aussems wanaibuka na pointi tatu basi watafikisha pointi 91 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote huku wakisaliwa na michezo miwili kutamataisha kipute cha msimu huu 2018/19.

Ugumu kwa mwenyeji kumzuia Mnyama ni wazi Simba wanahitaji kutangaza ubingwa leo kabla ya kwenda kuvaana na Sevilla ya Hispania mechi ya kirafiki inayotarajiwa kutandazwa Mei 23 pale Taifa jijini Dar es Salaam.

Faida kwa mwenyeji katika mechi ya leo ni kuweza kutumia uchovu wa Mnyama akitoka kumchachafya Ndanda FC kwa mabao 2-0. Na jana wakatumia kusafiri hadi kutua mjini Singida huku kichwani wakiwa na mchecheto wa kuwavaa Sevilla.

Simba akiwa kileleni na pointi zake 88, Singida ambao hawajawahi kupata ushindi mbele ya Simba tangu watue TPL ukiondoa sare waliopata katika mashindano ya Cecafa Kagame Cup ya 1-1 julai 4, 2018, wako nafasi ya 9 na pointi zao 45.

Kabla ya mchezo wa kesho rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara nne Simba wakishinda mara tatu na sare moja pekee huku kwenye Ligi wakiwa na ushindi wa asilimia 100 kila wanapokutana na Singida.

Katika michezo hiyo minne Simba walifanikiwa kupachika mabao 9 huku Singida wakifumania nyavu za Mnyama mara moja wakati kwenye TPL hawajawahi kupata hata bao dhidi ya Vinara hao.

Lakini pia ukitazama msimu huu takwimu zinaonyesha Simba wameshuka dimbani mara 35, wakishinda mechi 28, sare 4 na kupoteza mitanange mitatu tu.

Simba wamefanikiwa kufunga mabao 74 katika michezo hiyo 35, huku wakiruhusu mabao 14 pekee na kuwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi msimu hu una kufunga mabao mengi zaidi.

Kwa upande wa Singida tayari wameshacheza mechi 36 na kuvuna pointi 45, nafasi ya 9 kwenye msimamo wakifunga mabao 30 na kuruhusu 37 wakiwa na hasi ya mabao saba, wastani wa kufunga bao ni 0.8, huku 1.0 ni wakuruhusu nyavu zao kuchanika.

Simba, wastani wa kufunga mabao ni 2.1 katika kila mchezo wakati 0.4 ni uwezekano wa kufungwa bao katika kila mchezo.

Swali la msingi ni jinsi gani safu ya ulinzi ya Singida United itaweza kuzuia utatu mtakatifu wa washambuliaji wa Simba Medie Kagere MK14, John Bocco na Emmanuel Okwi walio funga mabao 52 kati ya 74 ya Simba.

Hapa kazi ipo kweli kweli ila mchezo wa soka huamuliwa na dakika 90 za mchezo husika.

Kuelekea mtanange huo viongozi wa pande zote mbili watema cheche huku kila mmoja akivutia kwake, kwa upande wa Simba
Ofisa Habari, Haji Manara amesema watashuka kwenye kandanda hilo wakihitaji pointi tat una si vinginevyo.

"Tunatambua mchezo wetu dhidi ya Singida United utakuwa mgumu ila tunachokwenda kukifanya kwa michezo yetu iliyobaki ni kushinda tu, hivyo Singida United wajipange kwa hilo.

"Tunajua kuna matokeo matatu kwenye mpira ambayo ni kushinda, kufungwa na kutoka sare sisi yote hayo hatutambui hesabu zetu ni kushinda tu," amesema Manara.

Nae Katibu Mkuu wa Singida United, Festo Sanga amesema kuwa wapinzani wao Simba wanapaswa watambue kwamba Namfua sio sehemu ya kutangaziwa ubingwa hivyo hilo walisahau.
"Kwenye msimamo tupo nafasi ya tisa ila kwetu sio salama, tunajua kwamba Simba wanahitaji pointi mbili ili kutangazwa ubingwa, nasi tunasema Namfua sio sehemu ya Simba kutangazwa kuwa mabingwa.

"Tumewekeza kwa ajili ya kushinda mchezo wetu, utakuwa mchezo wa jasho na damu pia tunatambua kwamba utakuwa mchezo wetu wa mwisho kucheza uwanja wa Namfua, lazima apigwe tu licha ya kwamba tunamheshimu.

"Tumejipanga kuona kwamba Simba anataga mayai matatu ikiwa na maana anaacha pointi tatu uwanja wa Namfua kivyovyote vile lazima akae uwanja wa Namfua kwa kuwa hatupo sehemu salama," amesema Sanga.

1 comment:

  1. Excеllent weƄlog here! Additionally ylur website so much uр fast!
    What host are you using? Can I get your affiliate
    link on your host? I wish my site loaded up as faѕ as yours lol

    ReplyDelete

Pages