July 10, 2019

COSTECH yatoa milioni 700 kwa wabunifu 60 kuendeleza tafiti na bunifu zao

Naibu Waziri wa  Elimu, Sayansi na Teknolijia, William Ole Nasha, akiwa katika banda la COSTECH  kwenye Monesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba'.
 Mkurugenzi Mkuu COSTECH, Amos Nungu, akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika viwanja vya Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF).


Na Tatu Mohamed, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetoa Sh. Milioni 700 kwa wabunifu 60 ili kuendeleza tafiti na bunifu zao na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.

 Akizungumza leo Julai 10, 2019 wakati wa kongamano maalum la Ubunifu lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa kushirikiana na COSTECH katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), Ole Nasha amesema Serikali itaendelea kuwatambua wabunifu na wagunduzi wa kazi mbalimbali nchini.

Amesema kwa sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na bunifu za kazi mbalimbali lakini zimeshindwa kutambulika na hivyo kuilazimu serikali kuanza kuweka utaratibu maalum ikiwemo kuandaa mwongozo unaotarajiwa  kuwatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali.

“Mwaka jana tuliandaa mashindano maalum ya ubunifu na walipatikana washindi wa kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalum wenye utaratibu wa kuendesha vituo vya teknolojia na ubunifu,” amesema Ole Nasha.

Aidha Ole Nasha ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuandaa kongamano la kila mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na  wabunifu hao kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kubaini kazi mbalimbali za wabunifu na watafiti na kuweza kutambulika.

Kwa mujibu wa Ole Nasha amesema wabunifu na wagunduzi nchini kutambua kuwa masuala ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na kuwataka wabunifu wasio katika sekta rasmi kuendelea kubuni bidhaa na vifaa mbalimbali kwa kuwa COSTECH si taasisi inayowagusa wasomi peke yao bali wabunifu wote waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.

Akifafanua zaidi Ole Nasha amesema kutokana na wabunifu na watafiti wengi kukabiliwa na changamoto ya kuibiwa kazi zao, aliitaka COSTECH kukaa pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA) ili kuhakikisha kuwa wabunifu wanawekewa utaratibu maalum kwa ajili ya kulinda bunifu zao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Prof. James Mdoe amesema serikali itaendelea kuzitambua kazi mbalimbali za wabunifu na wagunduzi nchini ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano madhubuti kwa ajili ya kutambua na  kuendeleza kazi za ubunifu na ugunduzi nchini.

Mkurugenzi Mkuu COSTECH, Amos Nungu amesema wataendelea kuwasaidia wabunifu wa ndani kuwa kuwapa nafasi ya kuonesha, kusikika na kuzielezea kazi zao katika maonesho mbalimbali. 

"Tunajua wapo wabunifu wengine shida yao si mitaji bali ni kusikika na kuonesha bidhaa zao, hivyo tunaimani maonesho haya yanawapa fursa wabunifu wetu kuelezea na kuonesha bidhaa zao, " amesema. 

Aidha Nungu ametoa wito kwa halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la kujenga kumbi za ubunifu katika maeneo yao, jambo litakaloimarisha upatikanaji wa maarifa na ujuzi mbalimbali kutoka kwa vijana.

Naye Mbunifu wa Maji taka kutoka Kampuni ya Biocon Africa Ltd, Prof. Karoli Njau ameitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wabunifu na wagunduzi wote nchini ili waweze kuonyesha kazi zao na kuhakikisha kuwa kuna utaratibu mzuri wa kuwapata watoa huduma katika kazi mbalimbali zinazoweza kupatikana nchini.

Katika mkutano huo,Wabunifu wawili kutoka mkoani Njombe wamekabidhiwa vyeti vya kuwatambua ambao Ni John Fute na Rainel Ngailo wakibuni mitambo ya kuzalisha umeme na kujenga kumbi ya ubunifu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kibunifu.

No comments:

Post a Comment

Pages