Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Bw. Leonard Nkamba wa kijiji
cha Kambanga wilayani Kasulu msaada wa sh. milioni 2.5 ili zimwezesha
kununua vitendea kazi vya kisasa vya kumsadia kufanya kazi yake ya
kuchonga vyombo mbalimbali vya mezani kwa kutumia miti. Makabidhiano
hayo yalifanyika mjini Kigoma Julai 24, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Kasulu, Kigoma
MKAZI wa
kijiji cha Kabanga wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Leonard Nkambam, anayejishughulisha
na uchongaji wa vyombo mbalimbali vya jikoni ameishukuru Serikali kwa kuanzisha
sera ya viwanda kwa kuwa imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ameyasema hayo
leo (Jumapili, Julai 14, 2019) baada ya
kukabidhiwa kiasi cha sh. milioni 2.5 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili aweze
kuongeza mashine itakayomuwezesha kuchonga bidhaa zenye ubora zaidi. Makabidhiano
hayo yamefanyika mjini Kigoma.
Bidhaa
anazochonga ni vikombe, chupa za chai, hot pot kwa kutumia mti aina ya
jakalanda. Mbali na kutengeneza vyombo hivyo, pia mjasiriamali huyo ambaye
ameajiri vijana watatu anachonga vibao na kuandika ujumbe mbalimbali kwa kutumia
unga wa ngano.
Akizungumza
baada ya kukabidhiwa fedha hizo na Waziri Mkuu, mjasiliamali huyo amesema
anaushukuru Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao uliona kazi zake na
kumuagiza atengeneze seti za vyombo kwa ajili ya zawadi za kumpelekea Rais Dkt.
John Magufuli.
“Uongozi wa
UWT mkoa wa Kigoma Taifa ulivutiwa na kazi zangu na kuniagiza nitengeneze chupa
ya chai, vikombe na hot pot kwa ajili ya kumpa zawadi Mheshimiwa Rais pamoja na
Waziri Mkuu ndipo Waziri Mkuu jana aliona kazi zangu na akavutiwa na bidhaa
ninazotengeneza ndipo akaniuliza kama kuna changamoto zinazonikabili nikamwabia
nahitaji mashine moja yenye thamani ya sh. milioni mbili na nusu akasema
umepata na leo sijaamini alivyoniita na kunikabidhi. Namshukuru sana.”
Nkamata
ametumia fursa hiyo kuwashauri wananchi wengine hususani vijana waache
kulalamikia suala la ukosefu wa ajira na badala yake wajiunge katika vikundi
vya ujasiriamali na kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo wataziuza na kujipatia
kipato.
Pia amewaomba
Watanzania wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na
viwanda vya ndani kwa kuwa vina ubora wa kutosha na pia watakuwa wanachangia
kukuza uchumi wa wajasiriamali na Taifa kwa ujumla. Amesema bidhaa
anazotengeneza ni rafiki wa mazingira kutokana na malighafi anazotumia.
Kwa upande
wake Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kujishughulisha na
shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili waweze kujipatia kipato na kuondokana
na umasikini. Pia amesema Serikali ipo tayari wakati wowote watakapohitaji msaada.
Waziri Mkuu
amempongeza mjasiriamali huyo kwa bidhaa
mbalimbali anazotengeneza ambazo ni nzuri na za kipekee. Amesemma amefurahi
kuona vikombe, chupa za chai pamoja na hot pot zilizotengenezwa na Mtanzania
kwa kutumia miti.
No comments:
Post a Comment