HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2019

Tigo yatoa kompyuta 20 MUST

Mkurugenzi wa Tigo, Nyanda za Juu Kusini, Henry Kinabo (katikati), akimkabidhi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Prof. Aloys Mvuma, moja ya kompyuta 20 zenye thamani ya Sh. Mil. 48 zilizotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya kuchangia masomo ya TEHAMA katika chuo hicho mkoani Mbeya. Kushoto ni  Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Ushauri na Utafiti, Prof. Godliving Mtui. (Na Mpiga Picha Wetu).


NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Tigo Tanzania imetoa msaada wa kompyuta 20 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Akizungumza baada ya kukabidhi kompyuta hizo, Mkurugenzi wa Tigo, Nyanda za juu Kusini, Henry Kinabo alisema wametoa msaada huo ili uweze kusaidia wanafunzi wa chuo hicho.

"Tunaamini ya kwamba kompyuta tulizozitoa hapa zitachangia sehemu kubwa katika kubadilisha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia zitaleta nafasi kwao kubuni teknolojia mpya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania," alisema.

Kinabo alisema Tigo ipo mstari wa mbele kwa ajili ya kuboresha viwango vya elimu katika vyuo vikuu kwa kuleta nyenzo za kusomea na kuwasaidia wanafunzi na walimu kukuza vipengele muhimu vinavyohitajika katika karne hii ya 21.

Alisema msaada huo ni juhudi zao za kuchangia malengo ya Serikali ya kuboresha na kuinua viwango vya elimu katika taasisi za elimu ya juu.

"Tumekabidhi kompyuta za mezani 20, zitakazo wanufaisha wanafunzi 4,630 wa MUST, ni imani yetu watazitumia vizuri ili ziweze kuleta mapinduzi ya kisayansi nchini," alisema.

Alisema kupitia mchango huo, Tigo imeunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika mtazamo wake wa kubadilisha nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo TEHAMA ndio chachu ya maendelea hayo.

Mnamo mwaka 2017, Tigo ilichangia kompyuta 47 katika Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), zilizo wanufaisha wanafunzi takriban 36,150. Mpaka leo jumla ya wanafunzi 40,780 katika vyuo vikuu nchini wamenufaika na msaada wa kompyuta kutoka Tigo kwa kipindi cha miaka miwili.

 Makamu Mkuu wa Chuo cha MUST, Profesa Aloys Mvuma, alisema msaada huo utasaidia kutoa stadi za kisasa za TEHAMA pamoja na maarifa kwa kizazi kijacho cha wataalam.

Alisema msaada huo utasidia nchi kukidhi mahitaji ya taarifa zinazobadilika mara kwa mara na mitindo ya kidigitali katika jamii na uchumi wa dunia.
Rasi wa Ndaki ya Sayansi na Elimu za Ufundi, Dk. John John, aliwashukuru Tigo kwa usaidizi wao mkubwa wa kompyuta hizo na kwamba  zitasaidia kuboresha kiwango cha elimu chuoni hapo.

"Tunawashukuru Tigo kwa kusaidia juhudi za serikali kwa kutoa mchango wa vifaa vya kufundishia masomo ya TEHAMA katika chuo chetu cha MUST.

 Tunaamini ya kwamba hizi kompyuta zitaboresha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia itaongeza ueledi katika elimu ya kidigitali hapa chuoni," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages