NA SULEIMAN MSUYA
HATMA ya mapendekezo
107 yaliyopendekezwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) itajulikana leo kupitia mkutano wa viongozi wakuu wa nchi 16
wanaokutana leo na kesho jijini Dar es Salaam.
Mapendekezo hayo
watawasilishwa kwenye Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC
utakaofanyika Agosti 17 na 18 jijini Dar es Salaam kwa uamuzi.
Nchi 16 zinazounda SADC
ni Tanzania, Malawi, DRC Congo, Namibia, Angola, Afrika Kusini, Shelisheli,
Mauritius, Comoro, Madagascar, Botswana, Eswatini, Zambia, Zimbabwe, Msumbiji
na Lesotho.
Akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kumalizika kikao cha mawaziri, Mwenyekiti wa
Baraza la Mawaziri la SADC, Profesa Palamagamba Kabudi alisema wao kama
mawaziri wanawajibika kupeleka mapendekezo kwenye vikao vya wakuu wa nchi ili
wafanye maamuzi.
Kabudi alisema baraza
hilo limekutana kwa siku mbili ambapo lilifanya majadiliano mapana na
kukubaliana kupeleka pamendekezo 107 mbele ya viongozi wakuu ili waweze kufanya
maamuzi kwa mujibu wa utaratibu wa SADC.
“SADC ina mifumo yake
ya kufanya kazi ambapo kamati zinakutana hatua kwa hatua hadi kufikia hatua ya
Marais hivyo haya mapendekezo 107 tuliyoyapitisha yanasubiria uamuzi wa Marais
wapitishe au wasipitishe,” alisema.
Kwa mujibu wa Kabudi
mapendekezo hayo moja linahusu SADC kukubali lugha ya Kiswahili kuwa lugha
rasmi ya nne ambayo inatumiwa na jumuiya hiyo katika vikao na mikutano.
Profesa Kabudi
akizungumza kuhusu Kiswahili, aliwashukuru wajumbe wa baraza kuona Kiswahili
kinafaa kupendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC na hatua hiyo inadhihirisha
kuthamini mchango Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika
ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
Profesa Kabudi alisema
Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi kwa wapigania uhuru, lakini pia
kinatumika kwenye nchi nyingi ikiwamo Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC,
Kaskazini mwa Zambia na inafundishwa kwenye vyuo vikuu 53 duniani.
Alisema Afrika Kusini
inaanza kukifundisha katika shule za msingi na sekondari hivyo ni wazi kwa siku
chache zijazo kitasambaa SADC nzima.
Alisema matarajio yake
ni kuona Rais John Magufuli ambaye anatarajiwa kupokea kijiti cha Uenyekiti
anahutumia kwa lugha ya Kiswahili iwapo viongozi wenzake wataridhia iwe lugha
rasmi ya SADC.
Kuhusu biashara ndani
ya SADC, alisema, “Nchi za jumuiya ziongeze biashara kati yao, kwani takwimu za
biashara zinaonesha iko chini sana kwa asilimia 20. Maana yake asilimia 80 ya
bidhaa zinatoka nje ya ukanda wetu. Tukiongeza biashara kati yetu tunaongeza
uwezo wa kutengeneza ajira”.
Kabudi ambaye ni Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alitaja mapendekezo mengine
kuwa kuhusu miradi ya maendeleo, vijana, jinsia na mengine mengi.
No comments:
Post a Comment