Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitazama chombo muhimu kinachounda mitambo ya kuzalisha umeme wa maji na gesi (turbine) wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni ya Toshiba nchini Japan jana. Wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Shinya Fujitsuka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa
Kampuni ya Toshiba nchini Japani, ambapo amewashawishi waje nchini na
wafungue ofisi kubwa na waanzishe viwanda vya bidhaa za elektroniki
watakavyoona vinafaa hapa nchini.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Agosti 27, 2019) baada ya kutembelea
Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza
mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni hiyo.
Akizungumza
na viongozi wa kampuni ya Toshiba, Waziri Mkuu amewashawishi waje
nchini na wafungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za
kielektroniki kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine
watakavyoona wao vinafaa kujengwa nchini.
Waziri
Mkuu amewahakikisha viongozi hao kwamba hawatojuta kuwekeza nchini
Tanzania kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji na
biashara pamoja na soko la uhakika wa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuwa
Tanzania imezungukwa na nchi nyingi.
“Wawekezaji
wote wanaokuja kuwekeza Tanzania wakiwemo na wa kutoka Japan pamoja na
kampuni ya Toshiba, watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha
mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika
wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo”.
Waziri
Mkuu amesema ujio wa kampuni kubwa kutoka nchini Japan utawapa
Watanzania fursa ya kujifunza tekinolojia mpya na namna bora ya
uendeshaji wa biahsara unaozingatia viwango vya Kimataifa.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri
amemwambia Waziri Mkuu kuwa Kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake
ya Tanzania na kufungua biashara, ambapo ameomba yafanyike mazungumzo
yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Mkutano wa Saba wa Tokyo International
Conference on Africa Development (TICAD 7) utakaoanza kesho Yokohama,
nchini Japan, amesema anaamini kuwa utakuwa na mafanikio makubwa
kutokana na ajenda zilizoandaliwa.
Waziri
Mkuu amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kuhusu
namna ya kuunganisha kibiashara shughuli za Serikali na sekta binafsi.
Amesema
kwa kutumia mkutano huo wa TICAD 7 wafanyabiashara wa Tanzania wanayo
fursa ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na makampuni makubwa ya
nchini Japan kama Toshiba ili kupata uzoefu na teknolojia muafaka.
Hivyo,
Waziri Mkuu amewasihi wafanyabiashara kutoka Tanzania ambao watashiriki
mkutano huo wafanye mazungumzo na wenzao wa Japan, wawashawishi ili
waweze kushirikiana nao kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.
Waziri
Mkuu yuko nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye
mkutano wa TICAD 7 utakaoanza kesho, ambapo ameambatana na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba
Kabudi na viongozi wengene wa Serikali na Taasisi za Umma.
No comments:
Post a Comment