*Nia yake ni wakulima waanze kulipwa
Jumatatu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza katika mkutano kwa njia ya video na Wakuu wa Mikoa inayolima Pamba ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara, Kagera, Singida na Tabora akiwa jijini Dar es Salaa leo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka
benki zilizoko kwenye mikoa inayolima pamba zihakikishe kuwa kesho Jumapili
zinatoa huduma kwa wateja ili wanunuzi wa pamba wakamilishe taratibu za mikopo.
“Kesho mabenki yanayotoa huduma Jumapili
ni vema yafanye kazi, ili wanunuzi wa pamba waje wakamilishe taratibu zote za
makaratasi na Jumatatu wapate hela ya kuanzia kazi. Hata mkifunga saa 6 mchana,
wao wabakie hadi saa 10 ili mradi wakamilishe taratibu zote,” amesema.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Agosti
3, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa nane inayolima
pamba ya Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga,
Singida na Tabora pamoja na Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.
Waziri Mkuu
amesema kikao kilichofanyika jana (Ijumaa, Agosti 2, 2019) baina ya Benki Kuu, wanunuzi wa pamba na wamiliki wa mabenki kimeafiki
kuanza kutoa mikopo kwa wanunuzi ili waanze kununua pamba kuanzia keshokutwa (Jumatatu,
Agosti 4, 2019).
Amesema kazi ya
kununua pamba ikianza, ilipwe kwanza iliyokusanywa ili ianze kusombwa na iweze
kupisha nafasi kwa pamba mpya itakayoendelea kununuliwa na kupelekwa kwenye
maghala.
Amemtaka pia Mwenyekiti
wa Wanunuzi, Bw. Christopher Gachuma ahakikishe anaweka ufuatiliaji ili kujua
kujua ni kiasi gani cha pamba kimenunuliwa kutoka kwa nani na wapi. “Endeleeni
na uratibu wa ununuzi mjue nani amenunua nini, wapi na kwa gharama ipi.”
Pia amewataka
wataalamu wa Wizara wa Kilimo waende mikoani, watu wa mabenki na Benki Kuu
washirikiane na taasisi ambata kama Bodi ya Pamba, Tume ya Ushirika na AMCOS ziratibu
vizuri kila mwananchi anayepeleka pamba na wahakikishe analipwa.
Wakati
huohuo,
Waziri Mkuu amewataka wanunuzi wa pamba na wafanyabiashara wote wajenge viwanda
hapa nchini ili kupata suluhisho la kudumu la soko la pamba. “Natoa wito kwa wafanyabiashara
nchini wajenge viwanda vya kusokota nyuzi na kutengeneza nguo.
Amesema hivi sasa nchini, kuna viwanda
viwili tu vya kusokota nyuzi ambapo kimoja kiko Dar es Salaam na kingine kiko
Shinyanga ambavyo uwezo wake ni mdogo. “Leo tumenunua pamba lakini tutaanza
kupata changamoto ya usafirishaji wa kuipelekea nje ya nchi kuiuza. Tukiwa na
viwanda hapa ndani, tatizo la soko halitakuwepo.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mabenki, Bw. Abdulmajjid Nsekela, aliwahakikishia
wakuu wa mikoa yote na wanunuzi waliokuwa wakishiriki mkutano huo kutoka kwenye
mikoa yao kwamba fedha itapatikana kuanzia Jumatatu (keshokutwa).
“Napenda
kuwahakikishia kuwa kwenye kikao cha jana, benki zote zimeridhia kwamba zitatoa
mikopo kwa wanunuzi. Tulikubaliana kwamba wanunzi wote walioomba mikopo waje
haraka kuchukua fedha zao, waliopata lakini wakawa hawajachukua mikopo waje pia
kuchukua.
“Mabenki yako
tayari kutoa fedha hizo, na tutasimamia ili kuhakikisha fedha zinatolewa kwa
wakati na wanunuzi wanapata hela,” alisema mbele ya Waziri Mkuu.
Naye Mwenyekiti wa Wanunuzi wa Pamba, Bw. Christopher Gachuma alisema
wanunuzi wako tayari kununua pamba ili itoke mikononi mwa wakulima iende kwa ginners (wenye vinu vya kuchambua pamba.
“Kuanzia wiki
ijayo, tutajitahidi kununua pamba kwa haraka na kwenye maeneo yasiyo na
wanunuzi tutakutana na kujipanga ili tuwafiie wote. Ila kwenye mikoa ya pembezoni
kama Katavi, ambako hakuna ginneries,
tunaomba upendeleo maalum sababu ya umbali uliopo.”
Naye Waziri wa Kilimo, Bw.
Japhet Hasunga amesisitiza kuwa wanunuzi wanaoenda kununua pamba wilaya za Meatu,
Igunga na Singida wawe makini na wapeleke kwenye ginneries maalum za kuchambua
mbegu na siyo za kusindika mafuta.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo ameiomba
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) isimamie kwa karibu makubaliano ya kikao cha jana
ili utekelezaji wake uende kwa haraka
zaidi.
“Ningeshauri Mwenyekiti wa Wanunuzi
afuatilie wafanyabiashara wake, ili wakipata hiyo fedha, waende wakatimize
malengo yaliyokusudiwa. Na Wakuu wa Mikoa mkutane na wanunuzi wa mikoa yenu
kila baada ya siku mbili, ili muweze kubaini kwa haraka changamoto
zinazowapata na kuzisuluhisha kwa haraka,” alisema.
No comments:
Post a Comment