Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Na
Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma
SERIKALI imeeleza kuwa itawalipa
waliokuwa wateja na wafanyakazi wa Benki ya FBME baada ya taratibu za kisheria
na majadiliano na Cyprus yatakapo kamilika hivi punde.
Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu
maswali ya Mhe. Jaku Ayoub, aliyetaka kujua Benki ya FBME ipo katika hali gani
na ni lini italipa wateja amana zao.
Dkt. Kijaji alisema kuwa wateja wa
Benki ya FBME waliokuwa na amana ya milioni 1.5 Serikali imewalipa kwa zaidi ya
asilimia 83 ya wateja wote, asilimia 17 iliyobaki ni ya wateja ambao
hawajajitokeza kuchukua amana hizo.
“Bodi ya Bima ya Amana (Deposit
Insurance Board- DIB) ilianza zoezi la kulipa fidia kwa mujibu wa sheria kwa
waliokuwa na amana katika benki hiyo kuanzia Novemba, 2017 na bado zoezi hilo
linaendelea”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa hadi kufikia Septemba 9,
2019 jumla ya kiasi cha Sh. milioni 2,404.2 kimelipwa kwa wateja 3426 kama
fidia ya bima ya amana, ambapo kiasi hicho ni sawa na asilimia 55.9 ya kiasi
chote kilichotarajiwa kulipwa kama fidia ya bima ya amana kwa wateja wote 6,628
waliopo Tanzania na wateja waliopo nje ya nchi (Tanzania International Banking
Depositors- TIB)
Aidha jumla ya Sh. milioni 2,401.2
zimelipwa, ikiwa ni asilimia 83.3 ya lengo la kulipa jumla ya Sh. milioni
2,882.6 kwa wateja waliopo Tanzania tu.
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango,
amempongeza Mwanasheria na Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Benki Kuu ya
Tanzania kwa kuhakikisha amana za wateja FBME ambao wako ndani na nje ya nchi
zinabaki salama na kuzipata baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa, Sheria ya Benki
na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 imeipa Benki Kuu ya Tanzania- BOT, mamlaka ya
kutoa leseni, kutunga kanuni, kusimamia benki zote zinazochukua amana za wateja
na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya benki zinazoendesha biashara bila
kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Kwa
ujumla Benki Kuu imepewa mamlaka ya kusimamia na kudhibiti benki na taasisi za
fedha ili kuhakikisha kuwa amana za wateja zinakuwa salama na pia kuna usalama,
utulivu na uthabiti wa sekta ya fedha na uchumi.
Benki ya FBME Ltd ilifutiwa leseni ya
kufanya biashara hapa Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania Mei 8, 2017 kutokana na
tuhuma za kujihusisha na biashara ya kutakatisha fedha nchini Marekani.
Benki
Kuu nchini Tanzania iliiteua Bodi ya Bima ya Amana- DIB kuwa mfilisi wa
Benki ya FBME, hivyo kwa sasa benki hiyo
haiendeshi shughuli zozote za kibenki hapa nchini.
No comments:
Post a Comment