Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango(katikati) akiwa na ujumbe wa Tanzania wakifuatilia
majadiliano na Benki ya Dunia kwenye Mkutano uliofanyika Jijini Washington DC.
Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington Dc
Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) ameiomba Benki ya Dunia-WB iwatume wataalam
wake nchini Tanzania ili waainishe miradi mikubwa ya kimkakati inayotakiwa
kutekelezwa kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP) badala ya taasisi hiyo ya Fedha
Duniani kutaka Serikali itekeleze miradi midogo isiyo na tija kubwa kwa Taifa.
Dkt. Mpango ametoa ushauri huo
Mjini Washington DC nchini Marekani baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem
ambapo aliwasilisha miradi mbalimbali ambayo Serikali inatekekeleza na ambayo
ameiomba Benki hiyo isaidie rasilimali fedha.
‘’Nisingependa kuona Taasisi
kubwa ya Kifedha kama Benki ya Dunia inakimbilia kufadhili utekelezaji wa vimiradi
vidogo vya kujenga hostel au hotel za nyota tano; Kwa sasa nchi yetu inahitaji
kujikita zaidi katika miradi mikubwa ambayo
itawaletea maendeleo ya haraka wananchi wetu’’ alisisitiza Mhe.Mpango.
Mhe. Mpango aliendelea kusisitiza
kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa na inayohitaji fedha nyingi
kuikamilisha, hivyo ni vyema Benki hiyo ikajielekeza katika kusaidia
utekelezaji wa miradi hiyo.
Dkt. Mpango alianisha miradi kama
ya Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius
Nyerere katika Mto Rufiji mkoani Pwani, Mradi wa Ujenzi wa Reli kutoka Mtwara
kwenda Mbamba Bay, Mchuchuma na Liganga ambako kuna rasilimali kubwa ya Madini
ya Chuma na Makaa ya Mawe.
Aidha Dkt. Mpango alisema katika
kutekeleza vyema miradi ya PPP Serikali imejikita katika mambo mawili moja ni
kuwa na programu ya kujenga uwezo kwa maana ya wataalamu wa kuitambua hiyo
miradi lakini pia, kuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina ili kujenga uwezo
wa majadiliano na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
‘’Nimewahimiza kwamba; kama kweli tunataka kutekeleza
kwa ufanisi mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP) ni
lazima tutekeleze miradi mikubwa, na kwa kuanzia, wangekuja kuanza kutekeleza
ule mradi wa kujenga reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbaba-Bay, Mchuchuma hadi
Liganga’’ alisema Mhe.Mpango.
Aliongeza kuwa ukamilishaji wa ujenzi wa reli hiyo
utasaidia kuchochea kwa kasi maendeleo ya nchi kutokana na rasilimali zilizopo katika maeneo
inapopita reli hii.
Dkt. Mpango alimshukuru Makamu wa Rais wa Benki ya
Dunia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem kwa kukubali maombi mengi kutoka
Tanzania ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment