HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2019

WANANCHI ARUSHA WAHIMIZWA CHANJO KWA WATOTO

Na Grace Macha, Arusha

WANANCHI Mkoa wa Arusha wametakiwa kuwapeleka  watoto wao wenye miezi tisa hadi miaka mitano kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali ili wapatiwe chanjo za magonjwa ya polio, surua na rubella.

Chanjo hiyo itaanza kutolewa  Oktoba 17 hadi 21 mwaka huu kwenye wilaya zote za mkoa huo ambapo kampeni hiyo imelenga kupunguza vifo kwa watoto wenye umri huo  vinavyotokana na ukosefu wa  chanjo.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Arusha, Azizi Sheshe (pichani), aliyasema hayo juzi wakati wa kikao cha uhamasishaji kuhusu  kampeni ya chanjo kwa wanahabari.

Alisema kuwa chanjo hizo zinatolewa na  Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto(UNICEF), na wadau wengine ambapo zoezi hilo linafanyika nchi nzima huku mkoani Arusha ikizinduliwa rasmi  wilayani Arumeru.

"Chanjo hizo zitatolewa kwenye hospitali, zahanati, vituo vya afya na maeneo yatakayochaguliwa kama baadhi ya ofisi za serikali za mitaa lengo ni kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa chanjo hiyo,"alisema Sheshe.

Alisema chanjo hizo sio za kupuuza kwa sababu zimesaidia kutokomeza magonjwa hayo kwa watoto ambapo mkoani Arusha ugonjwa wa polio haujaripotiwa kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, UNICEF, Dk.Thomas Lyimo aliwahimiza wananchi wawapeleke watoto wao wakapatiwe chanjo hiyo kwa sababu ni salama na inatolewa bure.

Alisema serikali na wadau wote wa afya wamejiridhisha kuwa chanjo hizo ni salama hivyo ni vema wazazi wakawapeleka watoto wote walengwa wenye umri wa miezi tisa hadi miaka mitano wapatiwe chanjo hiyo.

Mratibu wa Afya ya mzazi na mtoto Belinda Mumbuli aliwahimiza Waandishi wa Habari kutangaza chanjo hiyo ili wananchi wafahamu na kupeleka watoto wao.

Alisema katika utoaji wa chanjo hiyo ni bure  hivyo inapotokea kwenye kituo chochote kinachotumika kutoa chanjo hizo mtu akajaribu kuwatoza fedha wananchi wasisite kutoa taarifa kwao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika

No comments:

Post a Comment

Pages