Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akishirikiana na wafugaji kuingiza ng'ombe kwenye josho la Kijiji cha Kikonko wilayani Mlele mkoani Katavi wakati wa uzinduzi wa uogeshaji mifugo awamu ya pili na kutangaza ng'ombe mmoja sasa ataogeshwa kwa Sh. 50. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI wa Mifugo
na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua kampeni ya kitaifa ya uogeshaji mifugo
nchini na kutangaza neema kubwa kwa wafugaji ambapo sasa ng’ombe mmoja
ataogeshwa kwa shilingi 50 badala ya sh 500 huku Mbuzi na Kondoo
wakiogeshwa kwa sh 10 kila mmoja.
Uamuzi huu wa
Serikali utawawezesha kuokoa shilingi bilioni 19 ambazo wafugaji
wangezitumia kuogesha mifugo yao lakini ambapo sasa itatumika shilingi
bilioni 2.16 tu huku Serikali ikiwapatia wafugaji ruzuku ya asilimia 90
ambapo kama wafugaji wangeendelea na bei hiyo ya miaka ya nyuma
wangelazimika kutumia sh bilioni 21.6.
Akizungumza
mara baada ya uzinduzi wa Kampeni ya uogeshaji mifugo awamu ya pili
katika Josho la Kikonko wilayani Mlele na baadae mkutano mkubwa wa
hadhara uliofanyika Kijiji cha Majimoto, Waziri Mpina alisema kupitia
mpango huo Serikali itasambaza dawa ya ruzuku lita 12, 546 kwenye
majosho yanayofanya kazi 1,733 nchini kote.
Huku
Mvua kubwa ikinyesha kwenye mkutano huo, Waziri Mpina alitumia zaidi ya
saa moja kuhutubia huku akinyeshewa na mvua na kuwathibishia wananchi
kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuleta mageuzi kwa vitendo
hasa katika sekta ya mifugo.
Alisema Ilani ya
Uchaguzi ya CCM Ibara ya 25 kipengele inaiagiza Serikali kuhakikisha
mifugo yote inaogeshwa ili kuweze kuzuia magonjwa yote yanayoenezwa na
kupe ambapo asilimia 72 ya vifo vya mifugo vinasababishwa na kupe.
Hivyo
uogeshaji huo utawezesha mifugo kujikinga na maradhi na vifo ambapo
Serikali itaogesha michonyo milioni 38 kwa Ng’ombe, michonyo milioni 18
ya Mbuzi, michovyo milioni 7 ya Kondoo, na michovyo 2500 ya Punda hivyo
utaliwezesha taifa kupata mifugo bora ambayo haina magonjwa.
Waziri
Mpina alibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja Serikali
imekarabati majosho 400 na kwamba majosho yaliyobaki ambayo
hayajakarabatiwa ni 639 na kusisitiza kuwa yote yatakarabatiwa ili
kuongeza kasi ya uogeshaji mifugo.
Waziri Mpina
alisisitiza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu
yanasababishwa na mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa hivyo uamuzi
wa Serikali kuogesha mifugo pia umelenga kupambana na magonjwa kutoka
kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Hivyo juhudi
hizo zinapaswa kuungwa mkono na watendaji wote wa Serikali, wafugaji
wote ili kuboresha afya za mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya
mifugo ikiwemo nyama, maziwa na ngozi sambamba na kuwakinga wananchi na
maradhi yanayoweza kuambizwa kutoka kwenye mifugo.
Kufuatia
uzinduzi huo, Waziri Mpina ameagiza kila kijiji nchini kiwe na josho
kwenye vijiji vyote zaidi ya 12,000 ili kila kijiji kiweze kuogesha
mifugo na kusisitiza kuwa Serikali ya Rais Magufuli itakuja na mkakati
wa kuhakikisha kila kijiji kinapata josho kama sehemu ya kuboresha afya
za mifugo.
Pia ameziagiza halmashauri zote
nchini kuhakikisha majosho yote yamekarabatiwa ndani ya mwezi mmoja na
wizara itahakikisha inasambaza dawa kwenye majosho yote mabovu.
Aidha
amesisitiza wanaokwenda kuogesha mifugo wafuate sheria za uogeshaji
kuhakikisha mifugo inaogeshwa lakini kwa fedha ambayo Serikali
imeitangaza ya sh 50 kwa kichwa na ng’ombe na sh 10 kwa kichwa cha mbuzi
na zoezi hili litafanyika mfululizo kwa kipindi cha miezi 6 na
kumuagiza Mkurugenzi wa huduma za mifugo, Madaktari ya Mifugo wa Mikoa,
na Wilaya kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa vizuri kuhakikisha
wananchi hawatapeliwi
Pia Waziri Mpina ameweka
wazi kuwa Serikali itatangaza bei elekezi ya chanjo ifikapo 15 Novemba
mwaka huu na hakuna mtu mwingine atakayekwenda kuwaibia wafugaji tena na
kwamba chanjo ya homa ya mapafu ya ng’ombe itauzwa kwa sh 350 tofauti
na siku za nyuma ambapo walichanja kwa sh 2000 kwa kichwa cha ng’ombe.
Mkuu
wa Mkoa wa Katavi, Komredi Juma Homera amemhakikishia Waziri Mpina kuwa
Serikali ya mkoa huo inatasimamia maagizo yote na kwamba hakuna mfugaji
atakayeonewa au kudhulumiwa na kwamba bei elekezi iliyotangazwa ya sh
50 kwa kichwa ngombe na 10 kwa mbuzi italeta neema kubwa kwa wafugaji.
Pia
kuhusu malalamiko ya wafugaji kupigwa faini kubwa kuuawa kwa mifugo yao
amemkabidhi nyaraka za malalamiko hayo Kamanda wa Takukuru Mkoa wa
Katavi na kuwakamata watu wote waliotajwa na kuwafikisha kwenye vyombo
vya dola.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Wizara
ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Hezron Nonga amesema zoezi hilo la ugeshaji
litafanyika nchi nzima na kuwataka wafugaji kujitokeza kuogesha mifugo
yao ili kuikinga na maradhi.
No comments:
Post a Comment