NA SULEIMAN MSUYA, MOROORO
MAAKAMA ya Mwanzo Mikongeni, wilayani Mvomero mkoani Morogoro
Novemba 6 mwaka huu inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kujeruhi inayowakabili
wafugaji watatu Sperwa Kishakwii (16), Kashuma Kishakwii (18) na Daniel Babalai
(18) wanaodaiwa kuinigiza mifugo kwenye msitu wa hifadhi wa asili wa kijiji cha
Kihondo,
Kesi hiyo ilikuja
mahakamani Oktoba 30 mwaka huu kwa ajili ya ushahidi wa upande wa
wawalalamikiwa ambapo ushahidi wa pande zote mbili umekamilika ikiwemo ushahidi
wa mpelelezi wa kesi hiyo uliotolewa na Askari polisi mwenye namba G 4290 DC
Adonis wa Kituo cha Polisi Doma.
Akitoa ushahidi mahakamani hapo Mpelelezi wa kesi, alidai
kuwa mnamo Oktoba 8 mwaka huu saa 11 jioni alipokea taarifa ya kuwepo kwa
vurugu hizo kwenye kijiji cha Kihondo ambapo waliongozana na askari mwenzie DC-
Juma hadi eneo la tukio na kukuta vurugu zikiwa zimekwisha.
Alidai waliamua kwenda eneo lililokuwa na watu wengi kijijini
hapo na kubaini kuwepo kwa majeruhi wawili ambao ni Emmanuel Willnely aliyejeruhiwa kwa
kuvunjwa mguu wa kulia na Exavery Pius aliyejeruhiwa kichwani na mkono wa
kushoto.
Alisema majeruhi hao walikimbizwa Zahanati ya kijiji kwa matibabu
na kuhamishiwa Kituo cha Afya cha Kororo
ambapo baadae kupelekwa Hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro kutokana na
hali zao kutokuwa nzuri.
DC Adonis alidai mahakamani hapo kuwa baada ya majeruhi
kupelekwa hospitali alirejea ofisi ya mtendaji wa kijiji na kabla hajafika
alikutana na kundi la ng’ombe 179 ambao
hawakuwa na mchungaji huku wakifanana na 12 waliokamatwa awali ambapo alilazimika kuwaweka pamoja na kufikia
jumla ya ng’ombe 191.
Aidha alidai kuwa washtakiwa hao watatu walifika polisi siku
iliyofuata yaani Oktoba 10 mwaka huu na kutoa maelezo baada ya kuitwa kwa njia
ya simu kupitia kwa wazazi wao kufuatia wao kukimbia na siku iliyofuata Oktoba
11 mwaka huu kesi yao ilifikishwa mahakamani.
Mashahidi upande wa utetezi akiwemo mzazi wa mshtakiwa namba
1 na 3, Kishakwii Kailanga (45) alidai mahakamani hapo kuwa, wachungaji wake wa
ng’ombe wapo wawili ambao wote kwa pamoja walikwenda kuchunga siku ya tukio na
kwamba alipowahoji kabla ya kwenda polisi wamefanya nini walipotoka kuchunga
wadai hawakufanya chochote.
Aidha awali washtakiwa hao namba moja Sperwa Kishakwii (16)
na mshtakiwa namba tatu Kashuma Kishakwii (18) walidai mahakamani hapo kuwa
siku ya tukio hawakwenda kuchunga ng’ombe na badala yake walienda watoto
wengine waliopo nyumbani kwao na kuwataja kwa majina moja moja kuwa ni Nuhu na Leba.
Mshtakiwa namba mbili Daniel Babalai (18) alidai mahakamani
hapo kuwa siku ya tukio hakuwa mchungaji ambapo walichunga watoto wengine
ambapo yeye aliitwa polisi kukagua ng’ombe wake waliopotea baada ya ng’ombe
kukamatwa polisi na kisha kuwekwa rumande.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo washtakiwa hao waliwajeruhi
kwa fimbo na marungu askari wa kamati ya ulinzi wa msitu wa asili wa Kihondo
uliopo kata ya Doma ambao ni Emmanuel na Exavery.
Hakimu wa Mahakama hiyo Mussa Lilingani alisema, amelazimika
kuahirisha kesi hiyo ya kujeruhi namba 155/2019 hadi Novemba 6 mwaka huu
itakapokuja kwa ajili ya hukumu na kwamba dhamana za washtakiwa zinaendelea
kuwa wazi.
No comments:
Post a Comment